KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 26, 2012

VODACOM WAPASUA JIPU


KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesema suala la kuwepo kwa kipengele cha upekee 'Exlusivity' katika mkataba wa udhamini wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara kati yake na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni la muhimu katika kuepuka migongano ya kimaslahi.
Mkuu wa Udhamini na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Kelvin Twissa alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Vodacom inajali na kuthamini maendeleo ya klabu za soka nchini na kwamba itaendelea kufanya hivyo kwa kutoa fursa zaidi zinazolenga kukuza kiwango cha uwekezaji katika soka kwa masilahi ya klabu na taifa kwa jumla.
Twissa alisema katika kutambua umuhimu wa kupanua wigo wa uwekezazi katika ligi kuu ya Vodacom na maendeleo ya klabu, Vodacom Tanzania ilikubali kwa moyo mkunjufu kuruhusu klabu kutafuta wadhamini wengine, ambao siyo kampuni zinazofanya baishara sawa na Vodacom.
Ofisa huyo alisema hayo wakati wa kikao cha pamoja kilichowakutanisha viongozi wa TFF, kamati ya ligi kuu na Vodacom Tanzania kilichofanyika mjini Dar es Salaam jana.
“Tunatambua na kuheshimu utayari wa kampuni zingine, ambazo zipo tayari kushirikiana na sisi katika kudhamini ligi kuu ya Vodacom, nasi tupo tayari kushirikiana nao na hivyo kuleta maendeleo ya mpira wa miguu nchini,”alisema Twissa.
“Vodacom Tanzania inajivunia kuwa wadhamini wakuu wa ligi hii, tumeamua kuboresha udhamini wetu kwa sababu tunatambua umuhimu wa michezo kwa taifa letu, sasa michezo si kwa ajili ya burudani tu bali imekuwa chanzo cha ajira na kuboresha maisha ya wanaojihusisha nayo,” aliongeza.
“Tunaziomba klabu zinazoshiriki ligi kuu, vyombo vya habari na umma kwa ujumla kutambua kuwa azma ya Vodacom ni kuona mpira wa miguu unasonga mbele zaidi na ndio maana tumekuwa katika udhamni huu kwa zaidi ya miaka saba tukipitia vipindi tofauti, lakini hatukuwahi kukata tamaa. Hivyo si vyema wakati huu soka yetu inapokua, tukaruhusu hali inayoweza kusababisha changamoto katika uwekezaji wa soka,”alisema
Twisa.
Aliongeza kuwa, Vodacom itaendelea kushirikiana na TFF, kamati ya ligi na wadau wengine wote wa mpira wa miguu nchini katika kukuza uwekezaji kwa kuzisaidia klabu kupata wadhamini watakaosaidia maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment