KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 26, 2012

KAMATI YA UCHAGUZI TFF YACHARUKA


KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imewaonya wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi katika vyama vya mikoa na vilivyo wanachama wa shirikisho hilo kuepuka kutoa lugha na matamshi yanayokiuka kanuni za uchaguzi.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Deogratias Lyatto alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, baadhi ya wagombea uongozi katika vyama hivyo wamekuwa wakikiuka kanuni za uchaguzi kwa kutoa matamshi mabaya dhidi ya wapinzani wao kupitia kwenye vyombo vya habari.
Lyatto alisema kufanya hivyo ni makosa kwa vile baadhi ya matamshi yanayotolewa na wagombea hao ama wapambe wao yanaingilia na kukiuka taratibu za uchaguzi.
"Kamati inawataka wagombea wote waheshimu na kuzingatia kikamilifu kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF, vinginevyo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha wagombea wote wanapata fursa sawa,"alisema.
Lyatto alisema ni makosa kisheria kwa wagombea na wapambe wao kutoa matamshi yanayolenga kuzishawishi kamati za uchaguzi kutoa maamuzi yenye mwelekeo wa kuwanufaisha dhidi ya wapinzani wao.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi, ibara ya 9, wagombea wa nafasi za uongozi katika vyama vya michezo vilivyo wanachama wa TFF wanapaswa kuzingatia misingi ya uadilifu wakati wote wa uchaguzi.
Tahadhari hiyo ya kamati ya uchaguzi ya TFF imekuja huku kukiwa na msuguano mkali kati ya wagombea waliokatwa kwenye uchaguzi wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kamati ya uchaguzi ya chama hicho.
Baadhi ya wagombea waliokatwa wameilalamikia kamati hiyo kwa kuwapitisha wagombea wasiokuwa na sifa na kuwaacha wale wanaoonekana kuwa tishio dhidi ya wagombea wanaobebwa.

No comments:

Post a Comment