LONDON, England
MANCHESTER United huenda ikapata pigo lingine la majeruhi, baada ya mshambuliaji wake nyota, Robin Van Persie kuumia vibaya katika mchezo wa kimataifa wa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2014.
Van Persie aliumia katika mchezo, ambao Uholanzi ilishinda mabao 4-1 dhidi ya Hungary. Nahodha huyo wa zamani wa Arsenal aliyejiunga na Manchester United majira ya kiangazi, anadaiwa kuumia vibaya mguu wake wa kulia.
Kocha Mkuu wa Uholanzi, Louis van Gaal alimtoa mshambuliaji huyo baada ya kuumia. Kocha wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amesema ana hofu kubwa ya kumkosa Van Persie katika baadhi ya mechi kutokana na kuumia vibaya.
Kuumia kwake ni pigo kubwa kwa Manchester United kwa vile tayari timu hiyo imemkosa mshambuliaji nguli Wayne Rooney, ambaye atakuwa nje ya uwanja hadi mwisho wa mwezi huu baada ya kuchanika paja.
Van Persie (29) tayari ameifungia Manchester United mabao manne katika mechi tatu alizocheza. Pia aliifungia Uholanzi mabao mawili iliposhinda Uturuki mabao 2-0 Ijumaa iliyopita.
Katika mchezo mwingine, Ujerumani ilishinda mabao 2-1 ilipovaana na Austria. Mabao ya Ujerumani yalifungwa na Marco Reus na Mesut Ozil, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti.
Nayo Ufaransa ilivuna mabao matatu dhidi ya Belarus katika mchezo wa kundi I, ikiwa ni mwanzo mzuri kwa kocha mpya Didier Deschamps.
Sweden ilishinda mabao 2-0 ilipovaana na Kazakhstan wakati mabingwa wa zamani wa Kombe la Dunia, Italia walishinda bao 1-0 katika mchezo wao dhidi ya Malta.
No comments:
Post a Comment