KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 17, 2012

UMRI WA LULU WAZUA UTATA MAHAKAMANI

MSANII nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' akitoka katika Mahakama ya Rufani leo baada ya kusikilizwa kwa maombi ya upande wa Jamhuri ya kuomba kupitiwa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam wa kukubali kufanyia uchunguzi umri wa msanii huyo. (Na Mpigapicha Wetu).



NA FURAHA OMARY WA UHURU
JOPO la Majaji watu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, limeshangazwa na mawakili wa upande wa Jamhuri na ule unaomwakilisha msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ kulumbana kuhusu umri halali wa msanii huyo.
Hali hiyo ilijitokeza jana mahakamani hapo, mbele ya Jopo hilo la majaji chini ya Mwenyekiti Jaji January Msoffe, wakati wa usikilizwaji wa maombi namba 6 ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) dhidi ya mjibu maombi Lulu. Majaji wengine ni Jaji Benard Luanda na Jaji Edwin Rutakangwa.
AG aliwasilisha maombi ya kupitiwa kwa uamuzi wa Jaji Dk. Fauz Twaib wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kukubali kufanyia uchunguzi umri wa msanii huyo. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba.
Mwanasheria Mkuu aliwasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi Faraja Nchimbi na Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro huku Lulu akiwakilishwa na Wakili Flugence Fungamtama, Peter Kibatala.
Wakili wa Serikali Mwandamizi Nchimbi alidai katika hati yao ya maombi ina sababu tatu, lakini wataangalia mbili ambapo ya kwanza msimamo wao ni kwamba uamuzi wa Jaji Dk. Twaib alioutoa Juni 11, mwaka huu, ulikuwa batili kwasababu ulishindwa kujielekeza katika misingi mbalimbali ya kisheria.
Alidai ubatili huo wanafikiri kuwa Mahakama Kuu ilijikosesha iliposikiliza pingamizi la awali la upande wa Jamhuri pamoja na kujiridhisha na hoja hizo kwamba maombi hayo hayakuwa sahihi ilipaswa kuyatumbilia mbali na kuacha taratibu nyingine.
Wakili huyo alidai wanaungana na mtazamo wa Jaji Dk. Twaib kwamba iwapo Mahakama ya Kisutu ilikuwa na mamlaka ya kuchunguza umri wa Lulu.
Baada ya kudai hayo, Jaji Msoffe alimhoji Wakili huyo :’ Hivi lengo lenu Mahakama ya Kisutu irudi kuchunguza umri wa Lulu ili iweje? Ikishagundulika ana umri mdogo, kesi iende Mahakama ya Watoto ambayo haina mamlaka ya kusikiliza shauri la mauaji.
Jaji Luanda alisema gumzo la kuja mahakami hapo kwamba Lulu ana miaka 17 au 18 kama mtu mzima kesi hii inasikilizwa Mahakama Kuu.
“Suala la umri linakuja hapa (Mahakama ya Rufani) kwa misingi gani na ili iwe nini?” alihoji Jaji Luanda na kuongeza kuwa suala la umri linakuja kama mshitakiwa ametiwa hatiani ili kuangalia adhabu ya kupewa kama kunyongwa au la.
Wakili wa Serikali Nchimbi alidai Mahakama Kuu haikutakiwa kwenda mbele zaidi kuzungumzia uamuzi wa Hakimu wa Mahakama ya Kisutu na kuamua kufanya yenyewe.
Kwa upande wa Wakili wa Lulu, Peter Kibatala, alidai wao wameomba kuchunguzwa kwa umri wa msanii huyo kwa ajili ya kulinda maslahi ya mtoto ambayo kwa mujibu wa sheria ni mapana.
Alidai kesi ya mauaji ambayo adhabu yake kubwa ni kunyongwa hivyo huwezi kuingiza suala la umri kwa namna yoyote hadi kuwe na namna ya kuingiza suala hilo.
Jaji Msofe alisema : “Mahakama ya Kisutu haiwezi kusikiliza shauri hili mpaka wakati wa maelezo ya mashahidi na baada ya hapo linaenda Mahakama Kuu ambapo kuna usikilizwaji wa awali ndipo hapo hayo yangekuja.”
“Ubishi wa umri katika kesi ya mauaji kama hii, ili iwe nini, mmebishana Kisutu, Mahakama Kuu na mpaka hapa Mahakama ya Rufani” alihoji Jaji Msoffe na Jaji Rutakangwa.
Kwa upande wa Jaji Luanda alihoji : “Mnataka kutuambia akiwa na miaka 17 hashitakiwi?” ambapo Kibatala alijibu kuwa anashitakiwa.
Jaji Luanda alisema hiyo si kesi ya kwanza kufikishwa mahakamani kwani kuna watoto ambao wanatuhumiwa kwa mauaji na kwamba kifungu cha 26 cha Kanuni ya Adhabu kinaelekeza kuangalia suala la umri wa mtoto wakati wa usikilizwaji au pindi inapotaka kutolewa adhabu.
Majaji hao walimhoji Wakili wa Lulu iwapo mabishano hayo yanamsaidia mteja wao ambaye yupo rumande wakati kwa muda huo shauri lingekuwa linaendelea Kisutu.
Alipoelezwa na Jopo hilo la Majaji kutoa msimamo wao baada ya kusikiliza hoja zote, Wakili Kibatala alidai kesi irudi Kisutu ili wakaendelee na taratibu nyingine.
Jaji Msoffe alisema wataenda kutafakari waliyoambiwa na watatoa uamuzi katika tarehe ambayo pande husika zitajulishwa.

No comments:

Post a Comment