'
Wednesday, September 26, 2012
YANGA YASALIMU AMRI KWA FIFA
KLABU ya Yanga imeahidi kuyafanyia kazi malalamiko ya mchezaji wake wa zamani, John Njoroge na Kocha Kostadin Papic yaliyowasilishwa kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepokea taarifa ya malalamiko hayo kutoka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
"Haya mambo hatukuwa tukiyajua, tumeyakuta kwa uongozi uliopita, lakini baada ya kupokea taarifa hizi, hatuna budi kuyashughulikia,"alisema.
Sanga alisema watahakikisha suala hilo linashughulikiwa kikamilifu ili kuiepusha klabu hiyo na hatari ya kufungiwa ama kushushwa daraja.
Papic amefungua mashitaka FIFA dhidi ya Yanga, akidai malimbikizo yake ya mishahara, inayokadiriwa kufika dola 12,300 za Marekani (sh. milioni 17) wakati Njoroge anatakiwa kulipwa sh. milioni 17 kutokana na klabu hiyo kukatisha mkataba wake kienyeji miaka mitatu iliyopita.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alikaririwa juzi akisema kuwa, walijaribu kuwasiliana na viongozi wa Yanga ili Papic asiwasilishe malalamiko hayo, lakini juhudi zao hizo hazikuweza kufanikiwa.
Yanga imetakiwa kuwasilisha vielelezo vyake FIFA kuhusu malalamiko hayo ya Papic, vinginevyo huenda ikakumbana na adhabu ya kushushwa daraja ama kuzuiwa kuajiri makocha wa kigeni.
Njoroge aliishtaki Yanga kwa FIFA na kushinda kesi yake iliyoamuliwa Januari mwaka huu na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha shirikisho hilo.
Ushindi wa Njoroge unamaanisha kwamba, iwapo Yanga itashindwa kumlipa mchezaji huyo, itapokonywa pointi katika mechi zake za ligi na kushushwa daraja.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment