'
Wednesday, September 26, 2012
MANJI AWACHIMBIA MKWARA MASTAA YANGA
MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yussuf Manji amewaonya wachezaji wasioitakia mema timu hiyo na kuwataka wafungashe virago mapema kabla ya kusubiri kutimuliwa.
Manji alitoa onyo hilo juzi alipokutana na wachezaji wa timu hiyo katika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Alisema wapo baadhi ya wachezaji, ambao kwa makusudi hawataki kujituma na hivyo kuidhoofisha Yanga, hivyo ni bora wajiondoe mapema badala ya kusubiri kuondolewa.
Manji alisema yupo tayari kumlipa mchezaji yoyote, ambaye hapendi kuendelea kuitumikia timu hiyo na atafanya hivyo bila ya kuwa na kinyongo naye.
Mwenyekiti huyo wa Yanga alisema ni bora kuwa na wachezaji wachache wenye mapenzi na moyo wa kuitumikia timu hiyo kuliko kuwa na mamluki.
Aliwataka wachezaji wa timu hiyo kubadilika kwa kujituma zaidi uwanjani ili timu hiyo iweze kufanya vizuri zaidi katika mechi zake zijazo za michuano ya ligi kuu ya Tanania Bara.
"Kama hamtaki kujituma, ama timu itafungwa kutokana na uzembe, aliyesababisha hali hiyo lazima aondoke,"alisema Manji wakati wa kikao hicho.
Kwa sasa, Yanga inashika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi nne baada ya kucheza mechi tatu. Ilianza ligi hiyo kwa kulazimishwa kutoka suluhu na Prisons mjini Mbeya, ikapigwa mweleka wa mabao 3-0 na Mtibwa mjini Morogoro kabla ya kuicharaza JKT Ruvu mabao 4-1 mjini Dar es Salaam.
Matokeo hayo yalisababisha uongozi wa klabu hiyo kusitisha mkataba wa kocha wake, Tom Saintfiet kutoka Bulgaria. Nafasi yake inashikiliwa kwa muda na aliyekuwa msaidizi wake, Fred Felix Minziro.
Yanga inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumapili kumenyana na African Lyon kabla ya kuvaana na watani wao wa jadi Simba, Oktoba 3 mwaka huu katika mechi itakayopigwa usiku kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment