KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 26, 2012

HAFSA KAZINJA: TANZANIA HAINA MWANAMUZIKI WA KIMATAIFA


MWANAMUZIKI nyota wa miondoko ya zouk nchini, Hafsa Kazinja amesema licha ya kuwepo kwa wanamuziki wengi nyota na wenye vipaji, bado Tanzania haijaweza kutoa mwanamuziki mwenye hadhi ya kimataifa.
Hafsa alisema hayo wiki hii wakati akihojiwa na mtandao wa Vijimambo akiwa katika ziara yake ya maonyesho kadhaa ya muziki nchini Marekani.
Mwanadada huyo alisema ni vigumu kwa Tanzania kumpata mwanamuziki mwenye hadhi hiyo kutokana na matatizo yaliyopo kwenye vyombo vya habari nchini.
"Vyombo vyetu vya habari ni tofauti na vilivyopo Kenya na Uganda. Havitazami aina bora ya muziki na mwanamuziki,"alisema Hafsa, ambaye alianza kung'ara kimuziki baada ya kurekodi kibao chake cha Presha, alichomshirikisha Banana Zorro.
Kwa mujibu wa Hafsa, mwanamuziki anapokuwa hasikiki kwa muda mrefu, haina maana kwamba ameishiwa,lakini huo ndio mtazamo wa baadhi ya vyombo vya habari vya Tanzania.
"Mara nyingi wanamuziki wanaotamba, baada ya muda fulani huwa wanawekwa pembeni. Kuna niliowakuta kwenye gemu, wakapotea, waliwekwa pembeni, lakini bado wana wapenzi wao,"alisema.
Hafsa alisema ni vigumu kwa mwanamuziki kuishiwa kwa vile bado ana kipaji na hiyo ni kazi yake, hivyo anapaswa kuendelea kuungwa mkono badala ya vyombo vya habari kumwonyesha kwamba ameishiwa.
"Nasikia hasira sana kulizungumzia jambo hili. Kuna wakati Juma Nature alionekana ameishiwa na hana jipya, lakini siku alipopanda stejini kwenye tamasha la fiesta, mashabiki walilipuka mayowe ya kumshangilia, hii inamaanisha kwamba bado anakubalika,"alisema Hafsa,
"Wanaosababisha hali hii ni watu wa vyombo vya habari. Sipaswi kuvilalamikia sana kwa sababu mimi binafsi nimejulikana kwa sababu ya vyombo vya habari,"alisema.
Katika mazingira haya, Hafsa alisema itakuwa vigumu kwa Tanzania kuwa na mwanamuziki mwenye hadhi ya kimataifa iwapo vyombo vya habari nchini havitasimama kidete kuwatangaza badala ya kuwabomoa.
Hata hivyo, Hafsa alikiri kuwa, kuibuka na kuzama kwa wanamuziki huenda kunatokana na kujisahau kwao na kujihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu, hivyo wanapaswa kubadilika.
Mwanamama huyo aliipongeza serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya wasanii nchini kwa kuanza kutoza kodi kazi zote za sanaa ili waweze kufaidi matunda ya jasho lao.
"Kusema ule ukweli, serikali inatupenda sana, kuna vitu ambavyo imeshaanza kuvifanya, tusubiri tuone,"alisema.
Hafsa alikuwa miongoni mwa wanamuziki waliopewa nafasi ya kutumbuiza wakati wa sherehe za siku ya Mtanzania zilizofanyika hivi karibuni kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Marekani. Katika sherehe hizo, alipata nafasi ya kuimba baadhi ya nyimbo zake zinazotamba kama vile Presha na Mashallah.
Alisema alijisikia furaha kupata nafasi hiyo kwa vile ilikuwa heshima kubwa kwake kutumbuiza mbele ya mabalozi wa nchi mbali mbali na pia baada ya kubaini kuwa nyimbo zake zinajulikana na kupendwa hata na watu wa nje.
Licha ya wasanii wengi wa Tanzania kujulikana katika baadhi ya nchi za Ulaya, Hafsa alisema hadi sasa hakuna cha maana wanachokipata kutokana na kazi yao.
"Wasanii wa Tanzania bado tunakabiliwa na matatizo mengi. Tunafanyakazi nzuri na kubwa, lakini hakuna tunachokipata,"alisema.
Kwa mujibu wa Hafsa, soko la muziki wa Kitanzania kimataifa bado siyo zuri na kwamba kujulikana kwa baadhi ya wasanii katika nchi za Ulaya kumetokana na wizi wa kazi zao za sanaa na si kununuliwa kwa wingi na mashabiki.
"Siwezi kulizungumza hili kwa sababu lina vipengele vingi. Inawezekana mashabiki wanakujua, lakini kwa sababu ya kupeana CD zenye nyimbo zako, hawanunui,"alisema.
Hafsa ameufananisha wimbo wake wa Presha kuwa ni sawa na Georgina wa Safari Trippers ama Kitambaa Cheupe wa King Kikii kwa vile hauwezi kuchujuka haraka. Alisema wimbo huo utaendelea kutamba kwa karne kadhaa zinazokuja.
Mwanamama huyo anavutiwa sana na uimbaji wa wanamuziki wakongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mbilia Bel na Tshala Muana pamoja na mtanzania, Stara Thomas, ambao amewaelezea kuwa ndio waliochangia kumfanya ajitose kwenye fani hiyo.
Kipaji cha Hafsa kilivumbuliwa na mmiliki wa Nyumba ya Vipaji (THT), Ruge Mutahaba baada ya kuvutiwa na kibao chake cha Mashallah, ambacho ndicho kilichobeba jina la albamu yake ya kwanza. Hata hivyo, kibao kilichotamba kwenye albamu hiyo ni Presha.
"Ni kweli wimbo ulionipa sifa ni Presha, lakini kwangu wimbo wa Mashallah ndio kila kitu kwa sababu ndio ulionifungulia njia,"alisema.
Hafsa alisema moja ya sababu zilizoufanya wimbo wa Presha kupata umaarufu ni kukiimba kwa kumshirikisha Banana. Alisema umaarufu wa kibao hicho ulitokana na ukongwe wa Banana katika fani ya muziki.
"Wimbo wa Presha ulipata umaarufu kwa sababu ya Banana. Alianza muziki kabla yangu. Unapomshirikisha mwanamuziki maarufu, siku zote yeye ndiye anayepata sifa. Lakini mwisho wa siku ikajulikana kwamba mimi ndiye niliyemshirikisha,"alisema.
"Kwa sasa nikishirikishwa na msanii ambaye si maarufu, watu wanaweza kudhani wimbo ni wa kwangu. Ndivyo muziki ulivyo,"aliongeza.
Hafsa alisema anapendelea sana kupiga muziki wa zouk kutokana na umri wake na pia kwa sababu ya kuvutiwa zaidi na Mbilia Bel na Tshala Muana.
"Kwa umri wangu, zouk ndio aina ya muziki unaonifaa na kunipendeza,"alisema.

No comments:

Post a Comment