'
Wednesday, September 26, 2012
MGUNDA AWALIZA COASTAL UNION
UONGOZI wa klabu ya Coastal Union ya Tanga umeeleza kusikitishwa kwake na uamuzi wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda na msaidizi wake, Habibu Kondo kutangaza kujiuzulu.
Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu kutoka Tanga juzi, Mwenyekiti wa Coastal Union, Ahmed Aurola alisema wamezipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.
Aurola alisema kujiuzulu ghafla kwa makocha hao kumeuweka uongozi kwenye njia panda kwa vile bado timu hiyo inakabiliwa na mechi ngumu za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Alisema ameshangazwa na uamuzi huo wa Mgunda na mwenzake kwa vile hakukuwa na uhusiano wowote mbaya kati yao zaidi ya shinikizo kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo kutokana na Coastal Union kutofanya vizuri katika ligi hiyo.
Coastal Union ilianza ligi hiyo kwa kuichapa Mgambo JKT bao 1-0 mjini Tanga kabla ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Prisons mjini Mbeya na kutoka suluhu na Toto Africans mjini Tanga.
Matokeo hayo yaliifanya Coastal Union ishike nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, sawa na Prisons na JKT Oljoro zinazoshika nafasi ya tatu na ya nne. Simba inaongoza kwa kuwa na pointi tisa ikifuatiwa na Azam yenye pointi saba.
"Siyo tu uongozi, ambao umeshtushwa na kusikitishwa na kuondoka ghafla kwa Mgunda, bali hata wachezaji nao wamepatwa na mshtuko mkubwa," alisema Aurola.
Kwa mujibu wa Aurola, tayari wameshaanza kufanya mazungumzo na kocha Hemed Morocco wa Mafunzo ya Zanzibar ili aweze kuchukua nafasi ya Mgunda.
Mbali na kufanya mazungumzo na Morocco, alisema uongozi umekutana na wachezaji na kuwataka wasahau yaliyopita, badala yake waweke mbele majukumu waliyonayo katika ligi.
"Uongozi unamshukuru Mgunda kwa mchango mkubwa alioutoa kwa Coastal Union, lakini kwa vile ameamua kujiweka pembeni, hatuna kinyongo naye, tunamtakia kila la kheri,"alisema.
Mwenyekiti huyo wa Coastal Union amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo na kuwataka wawe na subira kwa vile bado timu yao inao uwezo wa kufanya vizuri katika ligi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment