KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Simba, Milovan Cirkovic kutoka Serbia ametamba kuwa, ushindi walioupata dhidi ya Azam umedhihirisha kuwa, kikosi chake kimekamilika kila idara na wapo tayari kuanza kutetea taji lao keshokutwa.
Majigambo hayo ya Milovan yamekuja baada ya Simba kuichapa Azam mabao 3-2 na kutwaa Ngao ya Jamii katika mechi iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Simba ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1 hadi mapumziko, kabla ya kuzinduka katika kipindi cha pili kwa kusawazisha na kuongeza bao la ushindi.
Milovan alisema ushindi huo umedhihirisha kuwa, timu yake bado ni bora na anaamini moto waliouwasha kwa Azam utaendelea katika mechi zao zijazo za ligi kuu na hatimaye kutwaa taji hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, kocha huyo alikiri kuwa safu yake ya ulinzi ilishindwa kucheza kwa uelewano katika kipindi cha kwanza ndio sababu wapinzani wao walipata mabao mawili na kuongoza.
Alisema hakutarajia iwapo wangeweza kuwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam kwa vile aliwapa maelekezo wachezaji wake kucheza kwa umakini mkubwa ili kuepuka kufungwa.
"Lakini baada ya hapo tulionyesha uwezo wetu, kwa sababu ukitoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2, maana yake ni kwamba Simba ni timu nzuri,"alisema kocha huyo.
Aliwapongeza wachezaji wake wa safu ya ushambuliaji, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa na Haruna Moshi kwa kusema kuwa walicheza kwa umahiri mkubwa na kuwataka mabeki wa timu pinzani kukaa chonjo na moto wao.
Hata hivyo, Milovan alikiri kwamba walipata upinzani mkali kutoka kwa Azam, ambayo alikiri kwamba ni timu nzuri.
Kocha huyo alikataa kuizungumzia safu yake ya ulinzi, ambayo ilipwaya kipindi cha kwanza na kuruhusu mabao mawili. Beki wa kati Paschal Ocheing alilalamikiwa na mashabiki kutokana na kuwa mzito na kuchelewa kutoa maamuzi.
Beki huyo alitolewa kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Nyosso, ambaye alicheza kwa uelewano mkubwa na Shomari Kapombe na kupunguza kasi ya mashambulizi kutoka kwa Azam.
Katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki lukuki, Azam ilijipatia mabao yake kupitia kwa John Bocco na Kipre Tchetche. Mabao ya Simba yalifungwa na Daniel Akuffour, Emmanuel Okwi na Mwinyi Kazimoto.
Ushindi huo ulikuwa wa kulipiza kisasi kwa Simba kufuatia kuchapwa mabao 3-1 na Azam katika mechi ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame iliyochezwa kwenye uwanja huo mapema mwaka huu.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Azam, Boris Bunjak amewatupia lawama waamuzi wa mchezo huo kwa madai kuwa, waliwabeba wapinzani wao Simba.
Akizungumza baada ya mchezo wa juzi, kocha huyo maarufu kwa jina la Boca alidai kuwa, waamuzi hao, Martin Sanya, Omar Kambangwa na Ephron Ndissa walionyesha mapungufu na kuwapendelea waziwazi wapinzani wao.
Hata hivyo, Boca alikiri kuwa Simba ni timu kubwa na nzuri, lakini Azam ilicheza vizuri zaidi na kustahili kuibuka na ushindi.
No comments:
Post a Comment