KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 13, 2012

SAINTFIET ATANGAZA SILAHA ZA KUIANGAMIZA PRISONS

KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet ametangaza kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya mechi ya ufunguzi ya michuano ya ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Saintfiet alisema ameteua wachezaji hao kutokana na mazingira ya mechi hiyo na pia uwezo waliouonyesha katika mechi za hivi karibuni na michuano ya Kombe la Kagame.
Aliwataja wachezaji wanaotarajiwa kuondoka kesho asubuhi kwenda Mbeya kuwa ni makipa Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma abdul, Godfrey Taita, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
Aliwataja viungo kuwa ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nizar Khalfan, Shamte Ally na Simon Msuva wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Didier Kavumbangu, Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza.
Aliwataja wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao hawatasafiri kwa ajili ya mechi hiyo kuwa ni kipa Said Mohamed, Ladislaus Mbogo, Job Ibrahim, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega na Issa Ngao wa Yanga B, ambaye anakomazwa kikosi cha kwanza.
Kocha huyo kutoka Ubelgiji alikiri kuwa mchezo wao dhidi ya Prisons utakuwa mgumu kwa vile wapinzani wao watakuwa wakicheza kwenye uwanja wa nyumbani na mbele ya mashabiki wao, hivyo amejipanga vyema kukabiliana nao ili aweze kutimiza lengo la kuibuka na ushindi wa kwanza kwenye michuano hiyo.
"Nimeaandaa kikosi changu vizuri, lakini tayari kina uwezo wa kucheza uwanja wa aina yoyote,hivyo tutaingia Sokoine kwa lengo la kupambano na kusaka ushindi, hilo halina mjadala,"alisema kocha huyo.
Alisema wachezaji watakaobaki mjini Dar es Salaam wataendelea na mazoezi na kujiunga na wenzao baada ya kurejea kutoka Mbeya kwa ajili ya kujiandaa na mchezo mwingine wa ligi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

No comments:

Post a Comment