KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, September 3, 2012

KLABU KUTETEA PINGAMIZI ZA WACHEZAJI WAKE

Klabu zote zilizowekewa pingamizi za wachezaji kwenye usajili na zile zilizoweka pingamizi zinatakiwa kufika kwenye kikao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kitakachofanyika kesho (Septemba 4 mwaka huu).

Kikao hicho kitafanyika kwenye ofisi za TFF kuanzia saa 6 kamili mchana, na kitakuwa chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa.

Klabu ambazo zimewekewa/ kuweka pingamizi na zinatakiwa kuwepo kwenye kikao zikiwa na nyaraka zote kuthibitisha madai yao ni Azam, African Lyon, Flamingo, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Oljoro JKT, Polisi Mara, Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation, Simba, Super Falcon, Toto Africans, Villa Squad na Yanga.

PONGEZI KWA UONGOZI MPYA KRFA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Septemba 1 mwaka huu).

Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KRFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Kigoma.

TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya KRFA chini ya uenyekiti wa Omari Saleh Mkwarulo ambaye amechaguliwa kwa kipindi cha kwanza.

Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Kigoma kwa kuzingatia katiba ya KRFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.

Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya KRFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.

Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Omari Saleh Mkwarulo (Mwenyekiti), Issa Bukuku (Katibu), Ahmed Msafiri Mgoyi (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Mohamed Nassoro (Mwakilishi wa Klabu TFF).

Nafasi za Makamu Mwenyekiti na Katibu Msaidizi zitajazwa kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika baadaye baada ya waliogombea ambao hawakuwa na wapinzani kushindwa kupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.

No comments:

Post a Comment