KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 20, 2012

YANGA KILIO MORO


Na Abdallah Mweri, Morogoro

TIMU ya Yanga imeendelea kushindwa kuonyesha cheche zake katika ligi kuu ya Tanzania Bara, baada ya kulambishwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Mtibwa Sugar ilistahili kutoka kifua mbele kutokana na kuidhibiti Yanga katika sehemu ya kiungo na kuwatumia vizuri winga Vicent Barnabas na mshambuliaji Hussen Javu walioipeleka puta ngome ya mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati 2012.
Viungo Shaban Nditi na Shaban Kisiga 'Malone' walitawala katika dimba la kati na kuisambaratisha Yanga ambayo imefanya usajili wa 'kufa mtu' kwa lengo la kufanya vizuri msimu huu.
Wachezaji mahiri waliosajiliwa na timu ya Yanga, Said Bahanuzi, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na Didier Kavumbagu, jana hawakufua dafu kwa Mtibwa waliocheza kwa jihadi katika dakika zote 90 za mechi hiyo.
Dalili za Mtibwa Sugar kutoka uwanjani na ushindi zilianza kuonekana mapema baada ya Barnabas na Javu kufumua mashuti ambayo yaliokolewa na kipa Ally Mustapha 'Barthez' ndani ya dakika 11 na kabla ya Dickson Mbeikya kufunga bao la kwanza kwa kichwa baada ya kujitwisha kona iliyochongwa na Malika Ndeule dakika ya 12.
Baada ya bao hilo Mtibwa walicharuka na kuwaweka roho juu mashabiki wa Yanga waliofurika Morogoro kutazama mechi hiyo ya pili kwa timu yao iliyoanza msimu kwa kupepesuka. Mechi ya kwanza ya ufunguzi wa ligi Yanga ilitoka suluhu na Prisons ya Mbeya katika Uwanja wa Sokoine.
Katika mechi ya jana ilifungwa bao la pili na Javu aliyetumia uzembe wa mabeki kujichanganya katika dakika ya 43, ambapo aliachia shuti la nguvu nje ya mita 18 kwa mguu wa kushoto na mpira kujaa wavuni ukimpita Barthez aliyeruka bila mafanikio.
Ngwe ya kwanza Yanga walionyesha uhai pekee katika dakika ya 19, 22 na 25 baada ya Hamis Kiiza, Bahanuzi na Frank Domayo kupiga mashuti ambayo yalipanguliwa na Shaban Kado, kipa ambaye Yanga imemrudisha Mtibwa Sugar kucheza kwa mkopo kutokana na kukosa namba.
Bao hilo la Mtibwa lilipatikana ikiwa dakika moja baada ya beki wake Ndeule kuondoa kwenye 'chaki' mpira wa kichwa kilichokandamizwa na Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Kipindi cha pili licha Yanga kuongeza nguvu mpya kwa kuwaingiza Didier Kavumbagu, Stephano Mwasika na Simon Msuva na kufanya mashambulizi butu kuanzia dakika ya 71, haikuweza kudhibiti kasi ya Mtibwa iliyokuwa mwiba kutokana na kuonana kwa pasi na kufika kwenye eneo la wapinzani wao kadiri walivyotaka.
Javu alihakikishia Mtibwa Sugar bao la tatu katika dakika ya 76 baada ya kufunga kwa kunyanyua mpira wa mbali wakati alipobaki ana kwa ana na Barthez.
Yanga ilicheza chini ya kiwango ikiwemo Kiiza kupaisha penalti iliyotolewa katika dakika ya 87 na mwamuzi Mathew Akrama wa Mwanza kutokana na beki Ndeule kuunawa mpira ndani ya kiboksi cha hatari.
MTIBWA: Shaban Kado, Malika Ndeule, Issa Issa, Dickson Mbeikya, Salvatory Ntebe, Shaban Nditi, Jamali Mnyate, Awadhi Juma, Hussein Javu, Shaban Kisiga na Vicent Barnabas/Ally Mohamed.
YANGA: Ally Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, David Luhende/Stephano Mwasika, Kelvini Yondani, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite/Didier Kavumbagu, Athuman Idd 'Chuji', Frank Domayo/ Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi na Hamis Kiiza.

No comments:

Post a Comment