KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 5, 2012

SIMBA, YANGA ZATUNUSHIANA MISULI

Beki Kevin Yondan anayegombewa na klabu za Simba na Yanga


Beki Mbuyu Twite kutoka Rwanda. Awali aliingia mkataba na Simba, baadaye akahamia Yanga


KLABU za Simba na Yanga zimeendelea kuonyeshana ubabe baada ya kila moja kugoma kufikia makubaliano kuhusu usajili wa wachezaji Kevin Yondan na Mbuyu Twite.

Viongozi wa klabu hizo wameamua kuonyeshana ubabe baada ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwataka wakutane na kufikia mwafaka kuhusu usajili wa wachezaji hao.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa ilishindwa kutoa uamuzi kuhusu pingamizi zilizowekwa kwa wachezaji hao baada ya Yanga kugoma kulipa fidia kwa Simba hadi waombwe radhi.

Awali, kamati hiyo iliwakutanisha viongozi wa Simba na Yanga na kuwataka wafikie makubaliano kuhusu usajili wa wachezaji hao ili waruhusiwe kuchezea timu wanazozitaka.

Katika kikao hicho, Yanga iliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa wakati Simba iliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu' na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Pope.

Simba iliwasilisha malalamiko TFF ya kufanyiwa mchezo mchafu na Yanga kwa kumsajili Twite wakati wekundu hao wa Msimbazi wakiwa wameshaingia naye mkataba na kumlipa sh. milioni 35.

Katika kikao hicho, Simba ilikubali irudishiwe fedha ilizomlipa mchezaji huyo, lakini Yanga walisema hawawezi kufanya hivyo hadi waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage anayedaiwa kusema wanatumia 'fedha chafu za EPA'.

Katika utetezi wao, viongozi wa Simba walidai kuwa, kauli hiyo ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi kama ambavyo Yanga walivyomvalisha Twite jezi yenye jina la Rage.

Kutokana na hali hiyo ya kutokuelewana, viongozi wa Simba hawakuwa tayari kujadili suala la Yondan na kuitaka kamati ya Mgongolwa kutoa maamuzi kwa kufuata sheria na kanuni.

Simba pia iliwasilisha malalamiko kwa kamati hiyo ikipinga Yondan kusajiliwa na Yanga kwa madai kuwa, bado alikuwa na mkataba na klabu hiyo hadi mwaka 2013.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam jana, Sanga alisema wapo tayari kuilipa Simba fedha walizompatia Twite, lakini baada ya kuomba radhi.

"Pesa zipo, lakini inabidi hao Simba watuombe radhi au wathibitishe Yanga inatumia pesa chafu za EPA. Haya ni madai mazito, ambayo yakipelekwa mbele ya vyombo vya sheria, hawataweza kuyathibitisha,"alisema.

Kwa upande wake, Hans Pope alisema jana kuwa, hawapo tayari kuomba radhi kwa sababu pesa wanazodai ni haki yao.Hans Pope alisema madai ya Yanga kutaka waombwe radhi kwanza, hayahusiani na suala la Twite.

“Tulikuwa tayari kulimaliza suala hilo nje ya utaratibu kwa Yanga kuturudishia fedha zetu, lakini sio kwa masharti ya kututaka tuwaombe radhi,"alisema.

Hans Pope alisema uamuzi wao wa kutaka warejeshewe fedha hizo hauna maana kwamba wanaomba pesa Yanga, bali wanadai haki yao.

"Tunadai haki yetu, tumeweka pingamizi Mbuyu asichezee sehemu yoyote hadi arudishe fedha zetu. Sasa wanaopokuja na masharti ya kuombwa radhi tunashindwa kuwaelewa, na kama ni hivyo waache sheria ichukue mkondo wake,”alisema.

Hans Pope alisema kwa kuwa sheria zipo wazi, mchezaji atakayesaini klabu mbili tofauti kwa wakati mmoja, anatakiwa kufungiwa miaka miwili hivyo wanasubiri kuona TFF itachukua hatua gani.Kamati ya Mgongolwa inatarajiwa kutoa maamuzi kuhusu pingamizi zake Septemba 11 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment