KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 20, 2012

WAMENIDHALILISHA, LAKINI HAWANIWEZI-TID




BAADA ya kuwa kimya kwa muda kuhusu tuhuma za kutaka kumuua msanii mwenzake Ali Kiba, msanii machachari wa muziki wa kizazi kipya nchini, Khaleed Mohamed 'TID' amesema tuhuma hizo hazikuwa na ukweli wowote.
TID amesema anashindwa kuelewa kwa nini alizushiwa tuhuma hizo kwa vile hana matatizo yoyote na Kiba, hajawahi kugombana naye na ni mtu wake wa karibu.
Kiongozi huyo wa Top Band aliwahi kushikiliwa na kuhojiwa na polisi kwa siku kadhaa kutokana na kuwepo kwa tuhuma hizo kabla ya kuachiwa huru.
"Hii kesi nashindwa kuielewa. Mimi ni mtu mzima sana, halafu ukiniambia nina matatizo na Ali Kiba wakati hata sijagombana naye, sielewi,"alisema TID wiki hii alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM.
"Hivi mtu unakwenda kwa mganga, unataka kujibasti, halafu mganga anakwambia TID katoa ngoma kali, anataka kukuua, wewe unachukulia siriasi, hivi vitu ni vya kijinga sana, unatakiwa kufikiria kwa makini,"aliongeza msanii huyo, aliyewahi kutesa kwa kibao cha Zeze.
Kwa mujibu wa TID, baada ya kukamatwa na kuhojiwa, polisi walichukua namba yake ya simu kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kimawasiliano kuhusu tuhuma hizo, lakini hawakuweza kupata lolote la maana.
Alisema uchunguzi huo wa polisi ulibaini kwamba, hakuwahi kuzungumza lolote na Kiba ama mtu mwingine yoyote aliyetaka kumuua msanii huyo, hali iliyothibitisha kwamba tuhuma hizo zilikuwa za uongo.
TID alisema kwa fikra zake, anahisi mganga aliyemweleza Kiba maneno hayo, alifanya makosa makubwa kwa sababu katika maisha yake, hajawahi kuwaza kutenda dhambi kama hiyo kwa vile anajiamini kutokana na kipaji chake.
“Yeye kama anataka kuwa mkali kunizidi mimi, ajifue, atoe ngoma kali, lakini hakuna mtu anayemchukia, mimi nampenda sana na kama yeye anakataa mimi simpendi, kwa nini ameingia kwenye remix yangu na nimemuweka pale?" Alihoji TID.
Msanii huyo mwenye makeke alisema anahisi kuna baadhi ya watu wanaomchukia katika gemu, lakini alisisitiza kuwa hawamuwezi.
“Wanataka kuniweka ndani, wanataka kunifunga jela, lakini hawaniwezi," alisisitiza msanii huyo.
Akizungumzia kesi aliyofungiwa, TID alisema ni lazima ifike kwa mwanasheria mkuu ili aweze kuangalia iwapo ni halali au ya kubambikiwa.
"Nimepata taarifa kwamba imerudishwa baada ya kubainika kwamba haiwezi kuwa kesi kwa vile haina ushahidi wowote. Imeonekana kuwa ni vitu vya kufikirika, ambavyo mtu alipanga vifanyike. Kwa sababu wao walitaka iwe kesi, na mimi nitawafungulia kesi kwa kunidhalilisha,"alisema.

No comments:

Post a Comment