KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 26, 2012

YANGA ISIKURUPUKE KUAJIRI KOCHA MWINGINE WA KIGENI


KLABU ya Yanga wiki iliyopita ilitangaza kumtimua kocha mkuu wa timu hiyo, Tom Saintfiet kutoka Ubelgiji kwa madai ya tuhuma za utovu wa nidhamu uliokithiri.
Akitangaza uamuzi huo kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alizitaja sababu za kutimuliwa kwa kocha huyo kuwa ni pamoja na kuwa mkaidi wa kutii maelekezo ya uongozi na kushindwa kuthibiti nidhamu kwa wachezaji.
Alizitaja sababu zingine kuwa ni kocha huyo, aliyekuwa na mkataba wa kuinoa Yanga kwa miaka miwili, kukataa kambi, kukiuka maadili, kujibizana na viongozi na kuzungumza hovyo na vyombo vya habari.
Licha ya kutolewa kwa sababu hizo, kuna habari kuwa, sababu kubwa iliyomfanya kocha huyo atimuliwe ni kitendo chake cha kumfokea kiongozi mmoja wa juu wa Yanga baada ya kocha huyo kumtukana mbele ya wachezaji.
Kufuatia kukatishwa kwa mkataba wa Saintfiet, uongozi wa Yanga umemteua msaidizi wake, Fred Felix Minziro kuwa kocha mkuu wa muda hadi atakapoajiriwa kocha mwingine mpya kutoka nje ya nchi.
Mbali na kukatisha mkataba wa Saintfiet, uongozi wa Yanga pia umewafungashia virago aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa, Ofisa Habari, Louis Sendeu pamoja na meneja wa timu, Hafidh Saleh.
Nafasi ya Mwesigwa imechukuliwa kwa muda na katibu mkuu wa zamani wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako wakati nafasi ya meneja wa timu huenda ikachukuliwa na mchezaji wa timu hiyo, Sekilojo Chambua. Nafasi ya ofisa habari bado ipo wazi.
Kutimuliwa kwa Saintfiet kulipokelewa kwa mshtuko mkubwa na wadau wa michezo nchini, hasa ikizingatiwa kuwa, hana muda mrefu tangu alipoanza kuinoa timu hiyo, akirithi mikoba ya kocha wa zamani, Kostadin Papic.
Mbali na kutokuwa na muda mrefu Yanga, kocha huyo pia alishajiwekea rekodi nzuri, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo. Pia aliweka rekodi ya kuiongoza Yanga kushinda mechi zaidi ya nane, kutoka sare mbili na kufungwa mbili.
Lengo la safu hii si kuunga mkono ama kuulalamikia uamuzi wa Yanga kumtimua kocha huyo. Lengo ni kujadili ni athari zipi, ambazo timu hiyo inaweza kuzipata kutokana na kumtimua kocha huyo wakati ambapo ndio kwanza ligi kuu ya Tanzania Bara imeanza.
Ikumbukwe kuwa, tangu Saintfiet alipoanza kuinoa Yanga, amekuja na mfumo mpya na ambao tayari wachezaji wameshaanza kuuzoea na kuutumia katika mechi kadhaa walizocheza. Sasa iwapo atakuja kocha mwingine mpya katika kipindi hiki, ni wazi kuwa atakuja na mfumo wake mpya na itachukua muda mrefu kwa wachezaji kuuzoea na kuanza kuutumia.
Kutokana na ukweli huu, ni vyema uongozi wa Yanga usitishe mpango wa kuajiri kocha mwingine kutoka nje kwa sasa, badala yake imwache Minziro aendelee kukaimu nafasi hiyo hadi baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.
Hii ni kwa sababu Minziro ni kocha mzoefu na ameshawahi kufanyakazi chini ya makocha wengi wa kigeni, anaufahamu vyema mfumo uliokuwa ukifundishwa na Saintfiet na ana uwezo wa kuendelea nao hadi mzunguko wa kwanza utakapomalizika.
Kama uongozi wa Yanga unayo nia ya dhati ya kuajiri kocha mwingine wa kigeni, ni vyema ufanye hivyo baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, ili hata kama atakuja na mfumo mpya, aweze kuwa na muda wa kutosha wa kuufundisha kwa wachezaji na kuutumia katika mzunguko wa pili.
Uzoefu unaonyesha kuwa, Yanga imeshawahi kufanya mabadiliko ya makocha katikati ya ligi mara kadhaa na mara zote yamekuwa yakiwaathiri wachezaji kutokana na kufundishwa mifumo tofauti katika ligi ya msimu mmoja.
Mabadiliko pekee, ambayo hayakuiathiri timu ni pale alipotimuliwa Kondic na kulewa Sam Timbe kutoka Uganda na hii ni kwa sababu kikosi cha Yanga kilikuwa kinaundwa na wachezaji wengi wazuri ndio sababu kiliweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya bara na Kombe la Kagame.
Hivyo ni vyema viongozi wa Yanga wasifanye papara ya kuajiri kocha wa kigeni kwa sasa, badala yake wampe nafasi Minziro ya kuonyesha uwezo wake na pia yale aliyojifunza kutoka kwa makocha waliotangulia kama vile Papic, Dusan Kondic, Timbe na Saintfiet.

No comments:

Post a Comment