KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 13, 2012

KING MAJUTO: UIGIZAJI SASA BASI



BAADA ya kutesa na kudumu kwenye fani ya filamu, maigizo na vichekesho kwa takriban miaka 30, msanii mkongwe wa fani hizo, Amri Athumani 'King Majuto' ameamua kusema sasa basi.

Majuto amefikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa, umri wake umekwenda mno na haoni iwapo kuna faida kwake kuendelea kuigiza.

Kitu kingine kilichomfanya Majuto afikie uamuzi huo ni wasanii wa fani hiyo kutothaminiwa hapa nchini na kulazimika kuuza kazi zao kwa bei ya chini.

"Umri wangu umekwenda sana, sioni kama ni sawa kwangu kuendelea kung'ang'ania kuigiza,"alisema Majuto alipokuwa akihojiwa na mtandao wa filamucentral hivi karibuni.

"Jambo jingine ni kwamba wachekeshaji wa Tanzania hatuna thamani. Hakuna anayezijali na kuzipa thamani kazi zetu kama wanavyofanya wenzetu wa nje. Kwa maana hiyo ni bora nikavue samaki au kulima,"alisema msanii huyo aliyeanza kujihusisha na fani ya uigizaji tangu miaka ya 1980.

"Unapatana na msambazaji bei nzuri, lakini anakuja mwingine na kusema kazi yake anauza kwa bei ya chini, hii haiwezi kuwa biashara tena, ni bora nitafute kazi nyingine ya kufanya,"alisema.

Kwa mujibu wa Majuto, anatarajia kustaafu rasmi kazi hiyo ifikapo Novemba mwaka huu na baada ya hapo, hatarajii kuigiza tena.

Majuto (60) alisema miongoni mwa kazi anazotarajia kuzifanya baada ya kustaafu ni pamoja na kuwaongoza wanawe na wasanii wengine katika fani ya uigizaji na vichekesho.

Kwa watazamaji wa kipindi cha Comedy Show, kinachoonyeshwa kila siku za Alhamisi usiku, kupitia kituo cha televisheni cha Channel Ten, jina la King Majuto sio geni kwao.Ni mmoja wa wasanii wakongwe wa maigizo na vichekesho nchini, lakini akiwa bado na kipaji cha hali ya juu katika kutunga vichekesho vinavyoonyeshwa kupitia kipindi hicho.

Umahiri wa Majuto katika fani hiyo haukuanza miaka ya hivi karibuni kama watu wengi wanavyofikiria. Safari ya Majuto ni ndefu, ikiwa ni pamoja na kukutana na vikwazo vingi vilivyomkatisha tamaa na kumfanya ajiweke pembeni na fani hiyo kwa miaka kadhaa kabla ya kuamua kurudi tena ulingoni.

Kama fani ya maigizo na vichekesho ingekuwa ikiwatajirisha wasanii wa fani hiyo, basi Majuto angekuwa bonge la milionea.

Kabla ya kuanzishwa kwa vituo vya televisheni na wasanii kupata fursa ya kurekodi kanda za video, alikuwa ametunga zaidi ya maigizo 1,000, lakini hakuna chochote cha maana alichoambulia.

Alipewa jina la King Majuto kutokana na umahiri wake katika fani hiyo na pia kumudu vyema kucheza nafasi alizokuwa akijipangia.
Majuto amepitia katika vikundi vingi vya sanaa za maonyesho kama vile DDC Kibisa, Wazazi Dancing Troup na vinginevyo akiwa na Mzee Pembe, Mzee Uzegeni, Tomato na wengineo.

Akiwa ndani ya vikundi hivyo, alishirikiana navyo kuonyesha maigizo kwenye kumbi mbalimbali za burudani za mjini Dar es Salaam kama vile DDC Kariakoo, DDC Magomeni Kondoa, Super Mini- Temeke, Deluxe Bar na zinginezo.

Hata hivyo, kutokana na fani hiyo kutokuwa na manufaa makubwa kwa wasanii wake, Majuto aliamua kujiweka kando na kurejea nyumbani kwake Tanga kwa ajili ya kuangalia shughuli zingine za kufanya.


Kuanzishwa kwa vituo vingi vya televisheni nchini pamoja na wasanii wa fani hiyo kupata fursa ya kutengeneza kanda za video za vichekesho, ndiko kulikompa fursa Majuto ya kurejesha makali yake na pia kuanza kunufaika na fani hiyo.

Hadi sasa, Majuto ametengeneza kanda nyingi za vichekesho kupitia Kampuni ya Al-Riyami ya mjini Dar es Salaam. Baadhi ya kanda hizo ni pamoja na Inye, ambayo imepigwa marufuku kutokana na kukiuka maadili ya kitanzania.

Nyingine ni Ngoma kubwa, In the Court, Inye Plus na zinginezo, ambazo zimetokea kuwakuna mashabiki wengi wa fani hiyo kutokana na kujaa vichekesho vya kuvunja mbavu.

Akizungumza na Burudani mjini Tanga hivi karibuni, Majuto alisema anamshukuru Mungu kwamba fani hiyo kwa sasa imeyainua maisha yake, tofauti na miaka iliyopita.

Majuto alisema japokuwa sanaa ya maigizo na vichekesho imeanza kumlipa uzeeni, anamshukuru Mungu kwa kuweza kunufaika na kipaji chake kuliko angekufa masikini.

“Pamoja na misukosuoko yote niliyoipata kupitia sanaa ya vichekesho, namshukuru Mungu kwamba nimefanikiwa kujenga nyumba ya kuishi na pia ninamiliki magari mawili,”alisema.

Licha ya kukabiliwa na vikwazo vingi katika sanaa hiyo, Majuto alisema kamwe hakufikiria kuiacha kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa.

Majuto alisema pamoja na umri alionao, ana uwezo wa kuigiza nafasi zote, ikiwa ni pamoja na ya kijana wa kawaida, muhuni, mvuta unga na mzee.

Alisema anawashangaa watu wanaofikiria kwamba, atastaafu kazi hiyo hivi karibuni kutokana na uzee. Alisema watu hao wanasahau kwamba, hiyo ndiyo kazi aliyopangiwa na Mungu katika maisha yake.

“Nawashangaa, wanadhani nitaacha kuigiza leo au kesho, eti kwa sababu umri wangu mkubwa, mbona kwenye mashindano mbali mbali nawafunika,"alisema Majuto.

Lakini kwa sasa, Majuto ameamua kuachana na msimamo wake huo baada ya kuona kuwa, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiwatumia kujinufaisha na kuyaacha maisha yao yawe ya kawaida.

Msanii huyo mkongwe alisema, ameshiriki kwenye mashindano mengi ya vichekesho na kuibuka na ushindi, lakini kamwe hajawahi kupewa zawadi zilizoahidiwa na waandaaji.

Kutokana na kutapeliiwa huko, Majuto alisema kamwe hatarajii kushiriki tena katika mashindano ya aina hiyo kwa sababu amebaini kuwa, waandaaji huyaandaa kwa lengo la kuwatumia kujinufaisha.

King Majuto anao watoto na wajukuu kadhaa, lakini hapendi kutaja idadi yao. Alisema hayo ni mambo yanayohusu maisha yake binafsi.

No comments:

Post a Comment