KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, September 11, 2012

WAMBURA BADO AIPASUA KICHWA TFF

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 10 mwaka huu) ili kupitia na kutoa uamuzi/ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.

Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.

Suala la ugombea wa Michael Wambura katika FAMMichael Wambura aliomba uongozi katika Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM) katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo. Wambura hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya TFF. Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya kushughulikia shauri hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya TFF ambayo ilimpa haki ya kugombea.

Kutokana na mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa mwisho katika masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa Kamati ya Rufani kuhusu uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya TFF iliomba mwongozo wa kisheria kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji.

Kwa vile Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa moja wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliishauri Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala hilo.

Katika muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si vizuri chombo kimoja kikawa msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi kwenye uchaguzi husika.

Hivyo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo mawili kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili kiwepo chombo kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

Mapendekezo hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF. AU. Rufani zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na Kamati ya Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo kiwe chombo cha mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwasilisha malalamiko yao.

No comments:

Post a Comment