KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 26, 2012

OKWI AFUNGIWA MECHI TATU, ATOZWA FAINI 500,000/-


KAMATI ya ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia mshambuliaji Emmanuel Okwi wa klabu ya Simba kucheza mechi tatu za michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Mbali na kufungiwa, kamati hiyo imemtoza faini ya sh. 500,000 mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha kamati ya ligi kilichofanyika juzi chini ya mwenyekiti wake, Wallace Karia.
Wambura alisema Okwi amefungiwa kwa mujibu wa kanuni ya 25 (1) ya ligi kwa kosa la kumpiga kiwiko beki Kessy Mapande wa timu ya JKT Ruvu ya mkoa wa Pwani.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Okwi alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani. Simba iliibwaga JKT Ruvu kwa mabao 2-0.
Kufuatia kupewa adhabu hiyo, Okwi sasa atakosa mechi zingine mbili za ligi kuu dhidi ya Prisons na Yanga. Tayari mchezaji huyo ameshakosa mechi moja dhidi ya Ruvu Shooting.
Simba inatarajiwa kumenyana na Prisons keshokutwa katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kuvaana na watani wao Yanga kwenye uwanja huo Oktoba 3 mwaka huu.
Wakati huo huo, kamati ya ligi imemwondoa George Komba kwenye orodha ya makamishna wanaosimamia mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Wambura alisema jana kuwa, Komba ameondolewa kwenye orodha hiyo kutokana na upungufu uliojitokeza kwenye ripoti yake ya mechi kati ya Simba na JKT Ruvu.
Kwa mujibu wa Wambura, kamati hiyo pia imeziandikia barua za onyo klabu za Africal Lyon, Mtibwa Sugar, Simba na mwamuzi Ronald Swai kwa makosa mbali mbali.
African Lyon imepewa onyo kwa kwenda uwanjani na jezi tofauti na ilizozionyesha kwenye mkutano wa maandalizi katika mechi yake dhidi ya Simba, Mtibwa imeonywa kwa kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji wake katika mechi kati yao na Ruvu Shooting wakati Simba imeonywa kwa kosa la mashabiki wake kushangilia kupita kiasi.
Swai ameonywa kutokana na upungufu aliouonyesha katika mechi kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wambura, mchezaji Faustine Lukoo wa Polisi Morogoro na Katibu wa Oljoro JKT aliyemwagiwa maji na wachezaji wa Polisil, masuala yao ni ya kinidhamu hivyo yamepelekwa mbele ya Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi kwa ajili ya hatua zaidi.
Wakati huo huo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga leo anatarajiwa kukutana na waandishi wa habari katika kikao kitakachofanyika saa sita mchana katika makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo Ilala, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment