BENDI ya muziki wa dansi ya Manchester Musica imekamilisha kazi ya kurekodi nyimbo zake saba zitakazokuwemo kwenye albamu mpya.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Jerome Mponda alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, nyimbo hizo zimerekodiwa kwenye studio tofauti kwa lengo la kuzipa ladha na vionjo tofauti.
Alizitaja nyimbo hizo kuwa ni Urithi wa baba, Kijumbe wa mtaa, Jackline, Haraka haina baraka, JK, Pesa na Dakika sita.
Jerome alisema kwa sasa, bendi hiyo imeimarika zaidi kibiashara kwa kufanya maonyesho kwenye hoteli za kitalii na kumbi za kawaida.
Alisema kila siku za Jumamosi, bendi hiyo imekuwa ikifanya maonyesho yake kwenye ukumbi wa Garden Breeze uliopo Magomeni Morocco wakati Jumapili, hutoa burudani kwenye ukumbi wake wa nyumbani wa Manchester uliopo Mbagala, Dar es Salaam.
Mbali na kufanya maonyesho Jijini Dar es Salaam, Jerome alisema bendi hiyo imekuwa ikialikwa kufanya ziara katika mikoa mbali mbali nchini.
Aliitaja mikoa waliyotembelea kuwa ni Dodoma, Shinyanga, Tanga, Mtwara, Lindi, Arusha, Iringa, Mbeya na Morogoro.
Wanamuziki wanaounda bendi hiyo ni Hamisi Juma (drums), Selemani Hamad (solo na tumba), Rajabu Salum (besi), lawrebnce Lan (kinanda) na Godfrey Mkude (mwimbaji na kiongozi).
Waimbaji wa bendi hiyo ni Saidi Kosa, Yohana Zungu, Black na Anet waliojiunga hivi karibuni wakitoka Tanzania House of Talent (THT).
Wacheza shoo ni Jenifer Urio, Asia na Papa Rock waliojiunga kutoka Dodoma na Tunduma mkoani Mbeya.
No comments:
Post a Comment