KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 20, 2012

WAKUVANGA: HALI YA VENGU BADO TETE


HALI ya msanii Joseph Shamba 'Vengu' wa kikundi cha vichekesho cha Orijino Komedi bado si nzuri na hakuna uwezekano wa kurejea katika maonyesho ya kundi hilo hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa na kiongozi wa kikundi hicho, Issaya Mwakilasa 'Wakuvanga' katika mahojiano maalumu na mtandao wa Millardayo wiki hii.
Wakuvanga alisema Vengu alirejeshwa nchini hivi karibuni akitokea India alikopelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu, lakini kutokana na matatizo yake kuwa makubwa, hajapata nafuu.
"Ukweli niwe muwazi, kwa afya yake na tatizo alilonalo, tunazungumzia tatizo la mshipa wa fahamu, tunazungumzia kitu kinaitwa ubongo, hayo matatizo yanachukua muda mrefu sana,"alisema Wakuvanga.
"Ukizungumza, ukiwaambia watanzania kwamba atarudi hivi karibuni, unakuwa unajidanganya wewe na watanzania wenzako, ndio maana siku zote tunasema ukiwa na nafasi ya kumuombea mtu unayempenda, muombee, mi siwezi kuahidi kwamba labda atarudi mwezi ujao au mwaka ujao,” aliongeza kiongozi huyo wa Orijino Komedi.
Alipoulizwa iwapo watamtafuta mtu mwingine kwa ajili ya kuziba nafasi ya Vengu, Wakuvanga alisema wataendelea kutumia jina lake hadi mwisho wa kikundi hicho.
"Kwetu sisi iko tofauti kidogo. Sisi tumeapa, ndivyo tunavyoishi, tuko saba mpaka tunakufa,"alisema Wakuvanga.
"Kuongezeka kwa mtu, labda sisi tukae pembeni tuwatafute watu wengine, lakini tutaendelea kuwa saba, hata maeneo tunayoishi na jinsi tunavyoishi mara nyingi tunaishi tuko saba, akipungua mmoja bado tuko saba,” alisisitiza msanii huyo, ambaye ameamua kujitosa kwenye fani ya muziki.

No comments:

Post a Comment