'
Thursday, September 20, 2012
SIMBA RAHA TUPU
LICHA ya kucheza ikiwa na wachezaji pungufu, Simba jana iliendelea kuunguruma katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitungua JKT Ruvu mabao 2-0.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, imba ilijipatia mabao yake hayo mawili kupitia kwa kiungo Amri Kiemba na mshambuliaji Haruna Moshi 'Boban'.
Kiemba alifunga bao la kwanza dakika ya 47 kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Amir Maftah, ambao uligonga nguzo ya pembeni ya goli na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni.
Boban aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 72 baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Ramadhani Chombo, aliyeingia badala ya Daniel Akuffour, ambaye aliwatoka mabeki wawili wa JKT Ruvu na kutoa pasi kwa mfungaji aliyeukwamisha wavuni.
Matokeo hayo yameiwezesha Simba kuendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Azam yenye idadi hiyo ya pointi, lakini zikiwa zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba ililazimika kucheza muda mwingi wa pambano hilo ikiwa na wachezaji 10 baada ya mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani kwa kosa la kumpiga kiwiko beki Kessy Mapande wa JKT Ruvu.\
Simba ilikuwa ya kwanza kubisha hodi kwenye lango la JKT Ruvu wakati Emmanuel Okwi alipochomoka na mpira na kupiga krosi iliyomita kipa Shabani Dihile, lakini mpira ulitoka nje.
Dakika tano baadaye, Mrisho Ngasa aligongeana vizuri na Mwinyi Kazimoto, aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga, lakini shuti lake lilipaa juu.
JKT Ruvu ilijibu mapigo dakika ya 22 wakati Omary Chang'a alipopewa pasi na Hussein Bunu na kuingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Juma Kaseja.
Mwamuzi Andrew Shamba kutoka Pwani alilazimika kumwonyesha kadi ya njani Kazimoto wa Simba kwa kosa la kucheza rafu na kisha kutoa lugha chafu kwa mwamuzi.
Beki Amir Maftah nusura aifungie bao Simba dakika ya 30 baada ya kupewa pasi murua na Daniel Akuffour, lakini shuti lake lilimbabatiza beki Damas Makwaya na mpira kutoka nje.
Kipa Dihile wa JKT Ruvu alilazimika kufanyakazi ya ziada dakika ya 34 kuokoa shuti kali la Mrisho Ngasa, aliyekuwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga bao kabla ya kuokoa shuti lingine la Nassoro Cholo dakika ya 36 baada ya kutema shuti la kwanza.
Pamoja na kucheza ikiwa pungufu, Simba ilifanya mashambulizi makali kwenye lango la JKT Ruvu dakika ya 39 na 44 wakati Haruna Moshi alipopewa pasi akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake la kwanza liligonga mwamba wa goli na la pili liliokolewa na mabeki. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa suluhu.
Daniel Akuffour nusura aiongezee Simba bao la pili dakika ya 49 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa krosi kutoka kwa Kiemba, lakini kipa Dihile aliuwahi na kuokoa.
JKT Ruvu ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 51 na 56 wakati Mapande na Jimmy Shoji walipoingia na mpira ndani ya 18, lakini shuti la kwanza liliokolewa na kipa Kaseja wakati shuti la pili liligonga mwamba na mpira kutoka nje.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Cholo, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi, Daniel Akuffour/ Ramadhani Chombo, Mrisho Ngasa, Emmanuel Okwi.
JKT Ruvu: Shabani Dihile, Kessy Mapande, Stanley Nkomola, Damas Makwaya, George Minja, Ally Khan, Saidi Otega/Amos Kagisa, Jimmy Shoji, Omar Chang'a, Hussein Bunu na Credo Mwaipopo.
Solomon Mwansele ameripoti kutoka Mbeya kuwa, wenyeji Prisons na Coastal Union zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Coastal Union ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 30 kupitia kwa Jerry Santo kabla ya Prisons kusawazisha dakika ya 52 kwa bao lililofungwa na Freddy Chudu baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Coastal Union.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment