KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 13, 2012

JULIO: SITAKI TIMU LIGI KUU

KOCHA machachari wa soka nchini, Jamhuri Kihwelu 'Julio' hivi karibuni alikataa ofa ya kuifundisha timu ya Coastal Union ya Tanga, inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara, badala yake amesisitiza kuwa, anataka kujikita zaidi katika soka ya vijana. Katika makala hii iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, kocha huyo msaidizi wa timu ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 17, Serengeti Boys, anaelezea sababu mbali mbali kuhusu uamuzi wake huo.

SWALI: Hivi karibuni ulikaririwa ukisema kuwa, huna mpango wa kufundisha tena timu za ligi kuu, badala yake utajikita zaidi katika soka ya vijana, hasa kikosi cha Serengeti Boys, ambacho wewe ni kocha wake msaidizi. Hebu tueleze kwa nini umefikia uamuzi huo?
JIBU: Nimekuwa nikifundisha timu za ligi kuu kwa muda mrefu sasa. Na huko nimekutana na mambo mengi sana, mazuri na mabaya, ambayo nisingependa kuyaeleza kwa sasa.
Lakini kwa kifupi ni kwamba nimeamua kujiweka pembeni na timu hizo kwa sababu ninayo progamu nzuri ya kuibua na kukuza vipaji vya vijana, ambavyo vitakuwa msaada mkubwa kwa timu yetu ya taifa miaka ijayo.
SWALI: Au uligombana na viongozi wa Coastal Union ndio sababu umeamua kujiweka pembeni na ligi kuu?
JIBU: Kwenye soka kuna mizengwe mingi kila kukicha. Kocha anaweza kushutumiwa kwa mambo mengi, ambayo pengine hakuyafanya, lakini kwa sababu viongozi wanataka kuficha maovu yao, huwa wakiamua kumsingizia. Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba nimeamua kujiweka kando na mizengwe.Sipo tayari kufundisha timu yoyote ya ligi kuu, iwe Coastal Union, Simba au timu nyingine kwa sababu nimekuwa nikipewa jukumu hilo wakati hali inapokuwa mbaya.
SWALI: Je, una mpango wowote wa kwenda kusomea ukocha nje ya nchi ama kufundisha soka Falme za Kiarabu?
JIBU: Kwa sasa nina mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumsaidia kocha wa timu za vijana kuifundisha Serengeti Boys na kwa wakati huu tupo kwenye maandalizi ya pambano letu dhidi ya Misri, hivyo suala la kusoma ama kwenda kufundisha soka Falme za Kiarabu kwa sasa halipo.
Lengo langu kubwa ni kuhakikisha tunaitoa Misri na kufuzu kucheza fainali za Afrika. Naamini Mungu akituwezesha kupata mafanikio hayo, nitapanda chati na kwa kweli sioni kwa nini tushindwe kufanya hivyo. Maana yangu kubwa ni kwamba kwa sasa nafanyakazi na TFF.
Lakini kwa safari zangu za kule Falme za Kiarabu, bado zitakuwepo kwa sababu nimewapeleka watoto wangu kule, wanasoma na kucheza mpira, hivyo nina kila sababu ya kwenda kule kila ninapopata nafasi kwa ajili ya kuwajulia hali na wakati mwingine nikipata kozi nakwenda kusoma.
SWALI: Vipi maandalizi ya mechi yenu dhidi ya Misri, yakoje?
JIBU: Tunamshukuru Mungu kwamba kambi yetu inaendelea vizuri na tumepata ofa ya kwenda kuweka kambi mkoani Mbeya, ambako pia tutacheza mechi kadhaa za kirafiki na timu za huko. Tumeamua kwenda Mbeya kwa sababu hali ya hewa ya huko kwa sasa inafanana na ile ya Misri
Vijana wote wapo katika hali nzuri, wanashika vyema maelekezo ya makocha na ninaamini mambo yakienda vizuri, tutaweza kuwafunga Wamisri na kusonga mbele.
SWALI: Hivi karibuni yalijitokeza malumbano kati ya viongozi wa klabu za Yanga na Simba kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji kutoka nje. Una mtazamo gani kuhusu matukio ya aina hii?
JIBU: Binafsi huwa nikishangazwa sana na matukio ya aina hii kwa sababu hayana lengo zuri kwa mustakabali wa soka ya Tanzania. Sielewi viongozi wa klabu hizi mbili wanataka kutupeleka wapi.Tunao wachezaji wengi wazuri hapa nchini, kuliko hao wa kigeni, lakini wanapoamua kufanya vitu wanavyovitaka wao, huwa hawataki kusikia ushauri wa mtu.
Nadhani wakati umefika kwa viongozi wa Simba na Yanga kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao vya timu za vijana ili kuwaandaa kuwa wachezaji wa timu kubwa hapo baadaye. Tumeona hivi karibuni jinsi kikosi cha pili cha Simba kilivyotwaa Kombe la BankABC baada ya kuzishinda timu ngumu za Mtibwa Sugar na Azam. Sioni kwa nini viongozi wameshindwa kuwapandisha daraja vijana hawa, badala yake wanakimbilia kusajili wachezaji wa nje, ambao baadhi yao uwezo wao ni mdogo.
Katika miaka ya nyuma, Simba na Yanga zilikuwa na utaratibu mzuri wa kupandisha wachezaji kutoka vikosi vyao vya pili ama kusaka wachezaji kutoka mikoani kwa kuwahusisha viongozi wao wa matawi, lakini hivi sasa zimebadilika kabisa. Zinawajali zaidi wachezaji wa kigeni kuliko wazawa.
Sipingi kwamba wachezaji wa kigeni wanaleta changamoto nyingi kwa wazawa, lakini hatuna sababu ya kuwapa kipaumbele kwenye timu zetu. Tunapaswa kusajili wachezaji wachache kutoka nje ili kutoa nafasi kubwa zaidi kwa vijana wetu.
Tazama wachezaji kama vile Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima na Hamisi Kiiza, hawa ukiwaita wanasoka wa kulipwa hukosei kwa sababu wamekuwa wakidhihirisha hivyo kwa vitendo, tofauti na wachezaji wengine, ambao wameigeuza Tanzania kuwa jalala la wanaojiita wanasoka wa kulipwa. Wanachuma na kuondoka.
Pengine ni vizuri usajili wa wachezaji kutoka nje ukafanywa na makocha badala ya viongozi, ambao wamekuwa wakitumia nafasi hiyo kujipatia umaarufu wa pesa na uwezo badala ya kuziimarisha timu zao.
SWALI: Unadhani ni kwa nini wanasoka wa Tanzania wanashindwa kupata mafanikio wanapokwenda nje kucheza soka ya kulipwa?
JIBU: Tatizo kubwa huwa ni mazingira. Wanapokwenda nje, wanakuta mazingira ya huko ni tofauti na yale waliyoyazoea. Wanajiona kama vile wapo kwenye dunia tofauti. Hawana malengo kama ilivyo kwa wenzetu wa nje.
Wakati mwingine mfumo wa uongozi wa timu zetu nao umekuwa ukichangia kuua vipaji vya wanasoka wetu. Wanastaafu soka baada ya kucheza kwa muda mfupi, wengine baada ya kuchanganyikiwa kutokana na mambo fulani.
Utakuta mchezaji hajalipwa mshahara kwa miezi minne hadi mitano. Katika mazingira haya, si rahisi kwa mchezaji kuelekeza akili yake katika kucheza soka. Anawaza yeye mwenyewe atakula nini, anaiwaza familia yake inavyoishi wakati timu inapokuwa kambini na mambo mengine mengi.
Katika hali hii, ni rahisi kwa akili ya mchezaji kutoka kwenye soka na kuanza kufikiria maisha yake yatakuwaje. Hali hii humfanya mchezaji kushuka kiwango kwa kasi ya ajabu. Tatizo kubwa huwa ni viongozi kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi kuliko ya wachezaji.
Tatizo lingine ni wachezaji wetu kubweteka baada ya kulewa sifa wanapokuwa hapa nchini na kupata mafanikio kisoka. Wengi wanashindwa kutambua kwamba mchezo wa soka ni ajira, siyo burudani. Binafsi ningekuwa na umri kama wa Shomari Kapombe ama Mrisho Ngasa hivi sasa, ningeelekeza zaidi akili yangu kwenye soka. Ningetumia muda wangu mwingi kucheza soka ili niwe fiti muda wote.
Tazama wanasoka wenzetu wa nchi za Afrika Magharibi walivyo makini na soka. Wanacheza kwa malengo huku wakiwa na uchungu wa maendeleo. Wanalipwa pesa nyingi na baadhi yao ni mamilionea hivi sasa.Baadhi yao wameanzisha miradi kwao na kutoa ajira kwa vijana wenzao.
SWALI: Ungependa kutoa mwito gani kwa serikali katika kuendeleza soka?
JIBU: Kwanza napenda kuipongeza TFF kwa kurejesha utawala bora wa soka hapa nchini. Hivi sasa kila kitu kinafanyika kwa uwazi, tofauti na miaka ya nyuma. Kuna utulivu mkubwa ndani ya TFF na hata vyama vya mikoa na wilaya. Kwa hili, uongozi wa TFF, hasa rais Leodegar Tenga wanastahili pongezi za dhati.
Pia napenda kuipongeza serikali kwa uamuzi wake wa kurejesha michezo katika shule za msingi, sekondari na vyuo kwa sababu ndiko kwenye chimbuko kubwa la wanasoka kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kabla ya kusimamishwa.
Mwito wangu mkubwa kwa serikali ni kuiomba itoe nafasi kwa makocha wazalendo kwenda nje kujifunza michezo wanayofundisha ili waweze kwenda na wakati kwa vile michezo huwa inabadilika kila kukicha.Naamini wakipata nafasi hizo mara kwa mara, nasi tutaweza kwenda na wakati na kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment