KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, September 5, 2012

DANNY MRWANDA: SIJUTII KUACHWA NA SIMBA



MSHAMBULIAJI Danny Mrwanda aliyesajiliwa na klabu ya Simba kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kabla ya kuachwa, amesema hajutii uamuzi huo kwa sababu alitarajia kitu kama hicho kutokea.

Mrwanda amesema kilichosababisha aachwe kwenye usajili huo ni viongozi wa Simba kusikiliza kelele na ushauri wa mashabiki bila kutazama kiwango cha mchezaji.

Amesema kwa kawaida, viongozi wa klabu wanaposikiliza kelele za mashabiki ni rahisi kufanya maamuzi kwa pupa bila kutazama ukweli wa mambo.

Mrwanda alisema hayo mjini Dar es Salaam wiki hii, alipotakiwa kueleza mustakabali wake baada ya viongozi wa Simba kuamua kumwacha kwenye usajili kwa madai kuwa, kiwango chake kimeshuka.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars alisema si kweli kwamba kiwango chake kimeshuka, isipokuwa wakati Simba ilipomsajili, alikuwa mapumziko na hakuwa amefanya mazoezi kwa miezi miwili.

“Tatizo ni kwamba viongozi wetu hawatazami kiwango cha mchezaji, wakishasikia tu kelele za mashabiki, wanafanya maamuzi,”alisema.

Mrwanda alisema wakati viongozi wa Simba walipomfuata na kutaka kumsajili, aliwaeleza wazi kwamba hakuwa fiti na aliwaomba wampe muda zaidi ili ajiweke fiti.

Alisema hata walipotaka kuingia naye mkataba, aliwaomba wampe mkataba wa muda mfupi.Alisema kilichomshangaza ni kuona kuwa mara baada ya kuingia mkataba na Simba, viongozi waliamua kumsajili kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame wakati walipaswa kumpa muda zaidi wa mazoezi ili awe fiti.

“Nisingeweza kucheza katika kiwango changu cha kawaida kwa wakati ule kwa sababu mwili uliongezeka na sikuwa nimefanya mazoezi kwa miezi miwili. Nilinenepa sana,”alisema mshambuliaji huyo aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa katika klabu ya DT Long An ya Vietnam.

Pamoja na kutemwa na Simba, Mrwanda alisema bado anaamini kiwango chake kipo juu na ndoto zake ni kuendelea kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.

Mrwanda alisema kwa sasa anasubiri maelekezo kutoka kwa wakala wake, ambaye ndiye mwenye jukumu la kumtafutia timu ya kuchezea nje.

“Nina mambo mengi sana ya kufanya kwa sasa. Naweza kuondoka wakati wowote. Namsubiri wakala wangu,”alisema.

Akizungumzia nafasi ya wanasoka wa Tanzania kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi, alisema wengi wanashindwa kufanya hivyo kutokana na woga.

Mrwanda alisema Tanzania inayo hazina ya wachezaji wengi wenye vipaji kuliko wanaotoka katika nchi za Afrika Magharibi na Kaskazini, lakini tatizo kubwa walilonalo ni woga na kutojiamini.

“Wenzetu wana nia na wanapotaka kufanya kitu, wanakifanya kwa dhati. Sisi tunakuwa na woga kabla hata ya kuanza kufanya hicho kitu,”alisema Mrwanda.

“Mchezaji anapopata nafasi ya kwenda nje, akisikia kwenye hiyo timu kuna Mnigeria ama Mghana, anaanza kutetemeka na kujenga hofu na kujiuliza, ‘nitaweza kweli’. Huwezi kufanikiwa kama unajenga hofu,”aliongeza.

Mrwanda amekiri kuwa, soka ya Tanzania bado inakabiliwa na matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na viongozi wa klabu na vyama vya soka kutokuwa na upeo wa kuongoza.

Alisema viongozi wengi wa vyama na klabu za michezo nchini hawajui kanuni za uongozi wa soka na wengine wamekuwa wakiingia madarakani kwa sababu ya uwezo wao kipesa.

“Soka ya Tanzania inapaswa kuongozwa na watu wanaojua mpira. Haiwezekani kiongozi aingie madarakani kwa sababu ya uwezo wake kipesa. Kiongozi wa aina hii anapoondoka madarakani, ni rahisi kwa klabu kuyumba,”alisema.

Alisema pia kuwa, viongozi wanaowekwa madarakani na wanachama kwa shinikizo la pesa ni rahisi kuwasikiliza watu hao kwa kila wanachotaka kifanyike na hata kutoa maamuzi kulingana na matakwa yao.

Mrwanda alisema wakati umefika kwa soka ya Tanzania kuongozwa na watu wenye sifa na uwezo unaotakiwa badala ya kuwakumbatia matajiri, ambao alidai huweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.Mrwanda alizaliwa Aprili 6, 1983.

Alianza kung’ara kisoka alipokuwa akichezea AFC ya Arusha kabla ya kusajiliwa na Simba.Alianza kucheza soka ya kulipwa mwaka 2009 katika klabu ya Al Tadamon ya Kuwait kabla ya kuhamia Vietnam, ambako alijiunga na DT Long An.

Aliteuliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa mara ya kwanza mwaka 2006 na kuichezea katika michuano mbali mbali ya kimataifa, ilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil.

No comments:

Post a Comment