'
Wednesday, September 26, 2012
JANGWANI KUWA KITEGA UCHUMI CHA YANGA
UONGOZI wa klabu ya Yanga umepanga kulifanyia ukarabati mkubwa jengo la makao makuu ya klabu hiyo lililopo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kwa lengo la kuligeuza kuwa kitega uchumi.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, ukarabati wa jengo hilo utakwenda sambamba na ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa soka utakaokuwa na uwezo wa kuingiza watu 5,000 kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa habari hizo, tayari Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji ameshafanya mazungumzo na kundi la wazee na vijana wa klabu hiyo kwa ajili ya kupata baraka zao.
Kikao hicho kati ya Manji na wazee pamoja na vijana wa klabu hiyo kilifanyika juzi makao makuu ya klabu hiyo kabla ya mwenyekiti huyo kuzungumza na wachezaji.
Uchunguzi wa Burudani umebaini kuwa, lengo la Manji kutaka kuligeuza jengo la Yanga kuwa kitega uchumi ni kuiongezea mapato klabu hiyo badala ya kutegemea mechi za ligi na michuano ya kimataifa.
Manji aliwaeleza wanachama hao wa Yanga kuwa, baada ya ukarabati huo kukamilika, jengo hilo litakuwa na hoteli kubwa na ya kisasa na itakuwa ikikodishwa kwa timu zingine na watu mbali mbali kwa ajili ya kuongeza mapato.
Mwenyekiti huyo alisema, hata timu yaYanga itakapokuwa ikiingia kambini kwenye hoteli, italazimika kulipia huduma za malazi na chakula, badala ya kukaa bure.
Kuna habari kuwa, tayari mkandarasi ameshapatikana na kufikia makubaliano na uongozi kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo, ambao unatarajiwa kuanza wakati wowote.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, timu ya Yanga haitakaa tena kambini kwenye jengo hilo hadi ukarabati utakapomalizika.
Habari zaidi zinasema kuwa, eneo la jengo hilo la kitega uchumi litakuwa na maegesho ya magari yasiyopungua 1,000 na kazi ya ukarabati inatarajiwa kuanza mwezi ujao.
"Manji ametuambia kwamba, baada ya ukarabati wa jengo la kitega uchumi kumalizika, mtu yeyote atakuwa na uwezo wa kupanga hoteli na kutumia fursa zingine zitakazopatikana kwa malipo,"kilisema chanzo cha habari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment