Katika pambano hilo lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mashabiki lukuki, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam.
Kwa kawaida, pambano hilo hufanyika kila mwaka, wiki moja kabla ya kuanza kwa ligi, likizikutanisha bingwa wa msimu uliopita na mshindi wa pili.
Ratiba ya ligi hiyo, itakayodhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom inaonyesha kuwa, michuano hiyo itaanza rasmi kesho kwa timu zote 14 kushuka dimbani katika viwanja saba tofauti.
Katika mechi hizo za ufunguzi, Simba itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati watani wao wa jadi, Yanga watakuwa ugenini kuvaana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Katika mechi zingine, Polisi Morogoro itavaana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro; Mgambo JKT itamenyana na ndugu zao wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga; JKT Ruvu itaonyeshana kazi na ndugu zao wa Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam; Azam watakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wakati Toto Africans itamenyana na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ligi ya msimu huu itazishirikisha timu 14, kati ya hizo, 11 ni zile zilizocheza msimu uliopita na tatu mpya. Timu mpya ni Mgambo JKT ya Tanga, Polisi Morogoro na Prisons ya Mbeya.
Hata hivyo, Polisi Morogoro na Prisons si timu ngeni katika ligi hiyo. Ziliwahi kushiriki mara kadhaa miaka ya nyuma kabla ya kushuka daraja na kurejea tena msimu huu, zikichukua nafasi ya Moro United, Villa Squad na Polisi Dodoma.
Ushindani mkali katika ligi hiyo unatarajiwa kujitokeza kwa timu za Simba, Yanga na Azam, ambazo licha ya kunolewa na makocha wa kigeni, pia zinaundwa na wachezaji kadhaa nyota kutoka nje ya nchi.
Historia inaonyesha kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, taji la ligi hiyo limekuwa likinyakuliwa kwa kupokezana kati ya Simba na Yanga huku Azam ikionekana kulinyemelea kwa hamu kubwa. Azam ilishika nafasi ya tatu mwaka 2010 kabla ya kupanda nafasi ya pili msimu uliopita.
SIMBA
Ilitwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya 18 msimu uliopita, ikitofautiana na Azam kwa pointi tatu na kuwaacha mbali watani wao wa jadi, Yanga kwa tofauti ya pointi tano.
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, kikosi cha Simba kipo chini ya Kocha Milovan Cirkovic kutoka Serbia, ambaye alikiwezesha kupata mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kuichapa Yanga mabao 5-0 katika mechi ya mwisho ya ligi hiyo.
Simba itacheza ligi ya msimu huu bila ya nyota wake kadhaa wa msimu uliopita, akiwemo marehemu Patrick Mafisango, aliyefariki kwa ajali ya gari na kuzikwa kwao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Pia itamkosa beki Kevin Yondan, aliyejiunga na Yanga.
Baadhi ya nyota wapya watakaounda kikosi hicho ni pamoja na mshambuliaji Mrisho Ngasa, aliyetokea Azam FC, Abdalla Juma kutoka Mtibwa Sugar, Kigi Makasi kutoka Yanga, Salim Kinje kutoka AFC Leopards ya Kenya, Ramadhani Chombo aliyerejea kundini kutoka Azam.
Nyota wengine wapya wanaotarajiwa kuonekana kwenye kikosi cha Simba ni pamoja na mabeki Paschal Ochieng kutoka Kenya na Kimabil Keita kutoka Mali na mshambuliaji Daniel Akuffo kutoka Ghana.
Nyota wa zamani wa kigeni watakaoonekana tena kwenye kikosi hicho ni Emmanuel Okwi kutoka Uganda na Felix Sunzu kutoka Zambia.
Akizungumzia ligi hiyo, Milovan alisema kikosi chake kimejiandaa vyema ikiwa ni pamoja na kucheza mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya Nairobi City Stars, Sony Sugar na Sofapaka za Kenya, ambapo ilifungwa mechi mbili na kutoka sare moja.
Hata hivyo, Milovan alikiri kuwa safu yake ya ulinzi haipo makini na atalazimika kufanyakazi ya ziada kuisuka upya kabla ya ligi kuanza. Alisema mabeki wake hawachezi kwa uelewano mkubwa kama ilivyokuwa msimu uliopita.
YANGA
Itacheza ligi hiyo ikiwa chini ya Kocha Tom Saintfiet kutoka Bulgaria, aliyerithi mikoba ya Kostadin Papic.
Kocha huyo ndiye aliyeiongoza Yanga kutwaa Kombe la Kagame mwaka huu baada ya kuichapa Azam mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tangu alipoanza kuinoa Yanga, Saintfiet ameiwezesha kushinda mechi nane, kati ya hizo tano za Kombe la Kagame, mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Rayon Sport na Polisi ya Rwanda na zingine nne dhidi ya timu za ligi kuu.
Chini yake, Yanga imepoteza mechi moja ya Kombe la Kagame dhidi ya Atletico ya Burundi baada ya kuchapwa mabao 2-0.
Baada ya kufanya vibaya msimu uliopita, Yanga iliamua kuwatema nyota wake wawili, Kenneth Asamoah kutoka Ghana na Davis Mwape kutoka Zambia kwa madai ya kushuka kwa viwango vyao. Lakini iliamua kuendelea kuwa nao Hamisi Kiiza kutoka Uganda, Haruna Niyonzima kutoka Rwanda na kipa Yaw Berko kutoka Ghana.
Nyota wengine wapya watakaokuwemo kwenye kikosi cha Yanga ni pamoja na kipa Ally Mustafa, aliyesajiliwa kutoka Simba, mabeki Juma Abdul na David Luhende, Mbuyu Twite kutoka Rwanda, Nizar Khalfan aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa Canada na washambuliaji Saidi Bahanunzi kutoka Mtibwa na Didier Kavumbagu kutoka Burundi.
Saintfiet ametamba kuwa, kikosi chake kimekamilika katika kila idara na kitakuwa moto wa kuotea mbali katika ligi ya msimu huu kutokana na kuundwa na wachezaji wengi wenye vipaji vya kusakata kabumbu.
Kocha huyo amekuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wa Yanga kutokana na kutumia mfumo wa uchezaji wa kuwa na mabeki wengi nyuma kwa lengo la kuimarisha ulinzi.
Katika mfumo huo, mbali na kuwa na mabeki wanne nyuma, huongeza wawili wa pembeni, ambao pia hucheza kama mawinga.
AZAM
Kwa sasa ipo chini ya Kocha Boris Bunjak Boca kutoka Argentina baada ya uongozi kuamua kuvunja mkataba wa kocha wa zamani, John Stewart Hall.
Kikosi cha Azam kinaundwa na wachezaji wale wale walioichezea msimu uliopita, isipokuwa kipa Deugratius Munishi 'Dida' na mshambuliaji George Odhiambo 'Blackberry' kutoka Kenya.
Hata hivyo, kabla ya ligi kuanza, Azam iliamua kuachana na Odhiambo kwa madai ya tuhuma za utovu wa nidhamu. Nafasi yake bado ipo wazi hadi sasa.
Nyota wa kigeni wanaotarajiwa kung'ara kwenye kikosi hicho ni mshambuliaji Kipre Tchetche kutoka Ivory Coast na beki George Owino kutoka Uganda, ambaye misimu miwili iliyopita, aliichezea Simba.
Wachezaji wengine wanaotarajiwa kuing'arisha Azam ni mabeki Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Said Morad, Jabir Azizi, Ibrahim Mwaipopo, John Bocco na Salum Abubakar.
Licha ya kuwa mgeni katika ligi kuu, Kocha Boca amesema anajivunia kikosi chake kuwa pamoja kwa miaka mingi na kwamba, anaamini kitaendelea kucheza kwa uelewano mkubwa na kwa dhamira ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.
MTIBWA SUGAR
Ni miongoni mwa timu chache kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam zilizowahi kutwaa ubingwa wa ligi hiyo. Ililitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1999 kabla ya kulitwaa tena mwaka uliofuata, ikifuata nyayo za ndugu zao wa Mseto waliotwaa taji hilo mwaka 1975.
Mtibwa itacheza ligi hiyo msimu huu ikiwa chini ya Kocha mpya, Mecky Maxime, ambaye ni beki wa zamani wa timu hiyo na nahodha aliyedumu kwa miaka mingi kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars. Maxime amechukua nafasi ya Tom Olaba kutoka Kenya.
Kikosi cha Mtibwa kimeondokewa na nyota wake wengi, wakiwemo beki Juma Abdul na mshambuliaji Saidi Bahanunzi waliojiunga na Yanga, lakini Maxime ametamba kuwa hilo haliwezi kuwababaisha.
Mtibwa imeziba mapengo ya wachezaji hao kwa kuwasajili Shabani Kisiga kutoka El Itihad ya Oman na Ayoub Hassan Isiko kutoka Bull FC ya Uganda.
Maxime amesema Mtibwa ni timu inayozalisha wachezaji wengi vijana, hivyo kuondoka kwao mara kwa mara ni jambo la kawaida na wamelizoea.
Kocha huyo aliponda utaratibu wa klabu kongwe za Simba na Yanga kupapatikia kusajili wachezaji wa kigeni badala ya kuoandisha wachezaji wao kutoka vikosi vya pili.
COASTAL UNION
Ni timu iliyoonyesha maajabu ligi ya msimu uliopita baada ya kufanikiwa kujinasua kutoka nafasi za mkiani na kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili.
Kikosi cha Coastal Union kinanolewa na Kocha Juma Mgunda, ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, akisaidiana na Habibu Kondo.
Timu hiyo maarufu kwa jina la Wagosi wa Kaya, ilianza vibaya maandalizi yake ya ligi kuu baada ya kupoteza mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya Bandari ya Kenya, Polisi Morogoro na Yanga, lakini ikajiweka sawa na kuibuka na ushindi dhidi ya Mafunzo na Super Falcon za Zanzibar.
Kuvurunda kwa Coastal Union katika mechi zake za kirafiki nusura kupoteze vibarua vya Mgunda na Kondo, lakini uongozi ulikaa imara kuwatetea na kuweka msimamo kwamba hawataondoka.
Miongoni mwa nyota waliosajiliwa na timu hiyo ni pamoja na viungo Jerry Santo kutoka Kenya, Razack Khalfan na Selemani Selembe, ambao safu yao ya kiungo imekuwa ikicheza kwa uelewano mkubwa.
Mgunda alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, kuvurunda kwa timu yake katika mechi za kirafiki hakuna maana kwamba ni mbovu. Alisema mechi hizo zilimsaidia kubaini mapungufu ya wachezaji wake na kuyafanyia kazi.
KAGERA SUGAR
Kwa sasa Kagera Sugar inanolewa na Kocha Abdalla Kibadeni, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars. Anasaidiwa na Mrage Kabange, ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Simba.
Katika kuimarisha kikosi chao, Kagera Sugar imewasajili Wilfred Ojodale Ame na Benjamin Efe Ofuyah kutoka klabu ya FC Abuja ya Nigeria. Pia ilikwenda nchi jirani ya Uganda kucheza mechi kadhaa za kirafiki.
Kabange alikiri hivi karibuni kuwa, ligi ya msimu huu itakuwa ngumu kutokana na timu nyingi kujiimarisha kwa kusajili wachezaji wapya kadhaa.
Kocha huyo alisema mazoezi waliyoyafanya na mechi za kirafiki walizocheza, zimewasaidia kujua uwezo wa timu na kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
PRISONS
Ni moja ya timu zilizorejea ligi kuu msimu huu baada ya kushuka daraja miaka miwili iliyopita. Iliwahi kushika nafasi ya pili katika ligi ya msimu wa mwaka 2000 na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.
Prisons, inayofundishwa na Kocha Jumanne Chale, ilicheza ligi kuu kwa mara ya kwanza mwaka 1999 na imewahi kushiriki mara mbili katika michuano ya Kombe la Shirikisho, mwaka 2005 na 2009, lakini mara zote iliishia hatua ya awali.
Kwa kifupi hakuna asiyefahamu umahiri wa timu hiyo katika soka ya Tanzania. Ni timu iliyowahi kuwa tishio kwa vigogo Simba na Yanga, ndiyo sababu iliposhuka daraja msimu wa 2009-10, mashabiki wengi waliisikitikia.
Prisons ni miongoni mwa timu zilizotoa wachezaji wengi kwenye kikosi cha Taifa Stars na pia Simba na Yanga. Miongoni mwa nyota hao ni Primus Kasonzo, Shadrack Nsajigwa, Henry Morris, Ivo Mapunda, Hussein Mataka, Oraph Mwamlima, Osward Morris na wengineo kadhaa.
Kwa maana hiyo, Prisons imerejea ligi kuu ikiwa na uzoefu mkubwa, hivyo ni matarajio ya wapenzi na mashabiki wa soka nchini kwamba itakuja na changamoto mpya katika ligi hiyo badala ya kuwa msindikizaji.
POLISI MOROGORO
Timu hii inayonolewa na Kocha John Simkoko, si ngeni katika ligi hiyo. Iliwahi kushiriki kwa miaka kadhaa na kutoa upinzani mkali kwa vigogo vya soka nchini kabla ya kushuka daraja msimu wa 2008/09.
Kutokana na kuwa timu pekee ya Jeshi la Polisi iliyobaki kwenye ligi hiyo msimu huu, baadhi ya wachezaji wake wanatoka katika timu ya Polisi Dodoma, iliyoshuka daraja msimu uliopita.
MGAMBO JKT, OLJORO JKT, RUVU SHOOTING, JKT RUVU
Mgambo JKT ni timu ngeni kabisa katika ligi kuu, hivyo inakabiliwa na mtihani mgumu wa kudhihirisha kuwa haikupanda daraja kwa kubahatisha, bali uwezo wake halisi wa kisoka.
Kupanda daraja kwa Mgambo JKT, kumelifanya jeshi hilo kuwa na timu nne msimu huu, zingine zikiwa JKT Ruvu, Oljoro JKT na Ruvu Shooting.
Kwa upande wa Oljoro JKT, inanolewa na Kocha Mbwana Makatta na ilitoa upinzani mkali msimu uliopita kiasi cha kudhihirisha kwamba, inastahili kuendelea kuwepo ligi kuu na kuendelea kuwapa raha wakazi wa Arusha.
Mbwana ambaye amerithi mikoba ya Ali Kidi, alikaririwa hivi karibuni akisema wamejiandaa kufanya vyema katika ligi hiyo kuliko ilivyokuwa msimu uliopita.
Ruvu Shooting inanolewa na Kocha Charles Boniface Mkwasa, ambaye pia alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars kabla ya kutangaza kujiuzulu hivi karibuni.
Timu hiyo haina historia ya kutisha kwenye ligi kuu, lakini ni miongoni mwa timu zinazotoa upinzani mkali na kuifanya ligi ishindwe kutabirika.
Akizungumzia ligi hiyo, Mkwasa alikiri kuwa, kuondokewa na wachezaji wake wengi msimu uliopita kumepunguza makali ya timu hiyo, lakini aliahidi kuwa watapambana kufa na kupona dhidi ya timu zingine.
Nayo JKT Ruvu inanolewa na Kocha Charles Kilinda. Kama ilivyo kwa Ruvu Shooting, imekuwa ikitoa upinzani mkali kwa timu zingine na kuongeza ushindani,hasa kwa vigogo, Simba, Yanga na Azam.
Kilinda alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa, watashiriki kwenye ligi hiyo kwa dhamira ya kutoa ushindani badala ya kuwa wasindikizaji.
TOTO AFRICAN
Ni timu inayonolewa na Kocha Athumani Bilali. Imenusurika mara kadhaa kushuka daraja na kuponea katika tundu la sindano.
Kocha Bilali alisema hivi karibuni kuwa, wamefarijika kupata udhamini kutoka kwa kampuni moja ya mjini Mwanza na hilo litawaongezea ari wachezaji ya kufanya vizuri zaidi.
AFRICAN LYON
Inanolewa na Kocha Pablo Verez kutoka Argentina, lakini haina malengo ya kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo zaidi ya kuibua vipaji vya vijana na kuwauza nje.
MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
1965 : Sunderland (Dar es Salaam)
1966 : Sunderland (Dar es Salaam)
1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam)
1968 : Yanga
1969 : Yanga
1970 : Yanga
1971 : Yanga
1972 : Yanga
1973 : Simba
1974 : Yanga
1975 : Mseto SC (Morogoro)
1976 : Simba
1977 : Simba
1978 : Simba
1979 : Simba
1980 : Simba
1981 : Yanga
1982 : Pan African
1983 : Yanga
1984 : Simba
1985 : Yanga
1986 : Tukuyu Stars (Mbeya)
1987 : Yanga
1988 : Coastal Union (Dar es Salaam)
1989 : Yanga
1990 : Simba
1991 : Yanga
1992 : Yanga
1993 : Yanga
1994 : Simba
1995 : Simba
1996 : Yanga
1997 : Yanga
1998 : Yanga
1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2001 : Simba
2002 : Yanga
2003 : Simba
2004 : Simba
2005 : Yanga
2006 : Yanga
2007 : Simba (Ligi Ndogo)
2008 : Yanga
2009: Yanga
2010: Simba SC
2011: Yanga SC
2012: Simba SC
No comments:
Post a Comment