KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 13, 2012

YANGA YAKUBALI KUILIPA SIMBA

KLABU ya Yanga imesema ipo tayari kuilipa Simba dola 32,000 za Marekani (zaidi ya sh. milioni 33) ilizompatia beki Mbuyu Twite kutoka Congo kwa ajili ya usajili wa msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, watalipa fedha hizo kama walivyoagizwa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti, Alex Mgongolwa imeitaka Yanga kuilipa Simba fedha hizo katika muda wa siku 21 baada ya kubaini kuwa, beki huyo alipokea fedha hizo kutoka Simba.
Kwa mujibu wa Mgongolwa, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Twite, hivyo ni mchezaji wake halali, lakini kwa vile imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba, inapaswa kuzirejesha ndani ya siku 21.
Usajili wa beki huyo ulizua utata mkubwa baada ya Simba kudai kuwa, ilimpa fedha hizo baada ya kutia saini mkataba wa kuichezea timu hiyo katika msimu ujao wa ligi.
Hata hivyo, beki huyo aliamua kubadili uamuzi wa kujiunga na Simba na kubisha hodi Yanga, ambako alilipwa kitita cha shilingi milioni 65.
Kufuatia beki huyo kubadili mawazo, Simba iliamua kumwekea pingamizi kwa kamati ya mgongolwa ikidai kuwa, Yanga ilicheza mchezo mchafu. "Hatuna kinyongo na uamuzi uliotolewa na kamati, hivyo tutailipa Simba fedha hizo katika muda uliopangwa,"alisema Mwesigwa.
Katibu Mkuu huyo wa Yanga alikiri kuwa, matatizo yaliyotokea katika usajili wa msimu huu yamewapa fundisho kubwa, ambalo hawawezi kulirudia msimu ujao.
Alisema uongozi ulipoteza muda mwingi kufuatilia pingamizi za Twite na Kevin Yondan, zilizowekwa na Simba na hivyo kushindwa kufanya mambo mengi ya msingi.
"Nafikiri tutakuwa makini zaidi katika msimu ujao ili kuhakikisha matatizo hayo hayajitokezi tena,"alisema.

No comments:

Post a Comment