KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, September 20, 2012

K-One akatisha mkataba na Baucha Records


BAADA ya kuwa chini ya Kampuni ya Baucha Records kwa miaka mitatu, msanii anayechipukia katika muziki wa kizazi kipya nchini, Karim Othman 'K-One' ameamua kujitoa na kuanza kufanyakazi zake kwa kujitegemea.
K-One amefikia uamuzi huo baada ya mmiliki wa kampuni hiyo, Ally Baucha kushindwa kutoa albamu yake kama walivyokubaliana kwenye mkataba kati yao.
Kwa mujibu wa K-One, amerekodi zaidi ya nyimbo 12 katika studio za Baucha, lakini hadi sasa ameshindwa kumtolea albamu.
"Nimesikitishwa sana na hali hii, ndio sababu nimeamua kutosaini mkataba mwingine na kampuni ya Baucha Records kwa sababu sioni faida yoyote ya kuendelea kufanyakazi chini yake,"alisema K-One alipozungumza na Burudani mjini Dar es Salaam wiki hii.
Msanii huyo alisema tangu alipokuwa chini ya Baucha Records, wimbo wake pekee ambao ulisambazwa kwenye vituo vya redio na televisheni ni Yule, aliourekodi kwa kushirikiana na Maunda Zorro.
Alisema licha ya wimbo huo kumpatia sifa na umaarufu mkubwa na pia kukubalika kwa mashabiki, Baucha hajaweza kuzisambaza nyimbo zake nyingine kwenye vituo vya redio na televisheni.
"Nyimbo zangu nyingine nazo ni kali sana. Fikiria nimerekodi na Ali Kiba, Chege, Tundaman, Madee, Top C na Becka Suspender, lakini nyimbo zote bado zipo kabatini," alilalamika msanii huyo, ambaye pia ni mtaalamu wa mambo ya kompyuta.
K-One alisema haelewi ni kipi kilichomsibu Baucha na kumfanya ashindwe kutimiza makubaliano yao kwa vitendo, hali inayomfanya ajione mnyonge kwa sababu wasanii wenzake wengi wamekuwa wakimkubali kutokana na kazi zake.
Mbali na kushindwa kusambaza kazi zake kwenye vituo vya redio na televisheni, K-One alisema Baucha ameshindwa kumwandalia maonyesho ya muziki kwa ajili ya kutangaza kazi zake.
Alisema kwa sasa yupo huru kwa vile hafungwi na mkataba wa Baucha Records na kwamba ameshaanza mikakati ya kumsaka meneja mpya kwa ajili ya kusimamia kazi zake.
"Ni kweli Baucha alikuwa na mipango mizuri ya kuniendeleza, lakini sielewi ni kipi kilichomsibu. Labda mambo yake hayakuwa mazuri, huwezi kujua, maana siku zote alikuwa akinipa ahadi za subiri kidogo,"alisema.
K-One alisema amefanyakazi nyingi chini ya Baucha Records, lakini hakuna faida yoyote aliyoipata. Hata hivyo, alimshukuru Baucha kwa kuishi naye kama mdogo wake na kumsaidia katika mambo mengi madogo madogo.
"Namshukuru sana Baucha kwa sababu amenisaidia kwa mambo mengi. Tatizo pekee ni kwamba nimeshindwa kutimiza ndoto zangu chini yake,"alisema K-One.
"Lengo langu ni kuwa msanii bora. Nahitaji kuwa na meneja aliye makini na mwenye malengo makubwa zaidi kwa sababu uwezo nilionao kiusanii ni mkubwa,"aliongeza.
Nyimbo zingine za K-One, ambazo bado hazijatoka hewani ni Dhahabu aliourekodi na Kiba, Ole ole aliourekodi na Chege, Mniache aliourekodi na Tunda Man, Niwaambia aliomshirikisha Madee, Weekend special aliourekodi na Becka Suspender na Tatu bora aliourekodi na Top C.
K-One alianza kuchomoza kimuziki baada ya kuibuka na vibao vyake viwili vya mwanzo, vinavyojulikana kwa majina ya Bila wewe na Sema baby, alivyorekodi na Ney wa Mitego na Pasha. Alirekodi vibao hivyo katika studio za Brain Trust, zilizopo Temeke, Dar es Salaam kwa udhamini wa dada yake.
Mbali na kurekodi vibao vyake, K-One pia alikuwa akishirikishwa kuimba viitikio katika nyimbo za wasanii mbali mbali maarufu wa muziki hao. Baadhi ya wasanii hao ni JB wa kundi la Mabaga Fresh na Mood Kibra.
Vibao vingine vya awali vya K-One ni pamoja na Valentine, Kwa nini, Mpenzi sasa why na Fau.
K-One amewaomba mapromota wa muziki wa kizazi kipya kujitokeza kumsaidia kurekodi albamu yake kwa vile anazo nyimbo za kutosha, zikiwa tayari zimesharekodiwa. Amewahakikishia mapromota hao kwamba hawatajutia kutumia fedha zao kwa kazi hiyo.
Je, ni kwa nini K-Onea aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya?
“Tangu nikiwa mdogo, nilipenda sana kushiriki katika maigizo na shughuli zozote zilizohusu mambo ya muziki. Ndipo nilipojigundua kwamba ninacho kipaji cha muziki kwani tangu nikiwa shule, niliweza kutunga mashairi ya wimbo,”alisema.
Kwa mujibu wa K-One, katika familia yake, hakuna ndugu yoyote aliyewahi kujihusisha na muziki huo. Ni yeye pekee, aliyejitosa kwenye fani hiyo baada ya kubaini kuwa, ana uwezo nayo.
“Lengo langu ni kuwaonyesha watanzania kwamba nina kipaji cha muziki. Pia nataka niutumie muziki kama ajira yangu kwa sababu ni biashara inayolipa,”alisema.
K-One ametoa wito kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, wapendane, kusaidiana na kuaminiana ili waweze kupiga hatua za juu zaidi kimaendeleo.Alisema miongoni mwa sababu zinazochangia kuwakwamisha wasanii chipukizi wa muziki huo, ni kutokuwepo kwa umoja miongoni mwao, kuchukiana na kutosaidiana.
“Wasanii walio juu wanapaswa kukumbuka kuwa, kabla ya kufika huko waliko hivi sasa, nao walianzia chini, hivyo wasikwepe kuwasaidia wenzao wanaohitaji msaada kutoka kwao, hata kama wa kurekodi pamoja,”alisema.

No comments:

Post a Comment