Timu ya soka ya Yanga jana iliichapa Coastal Union mabao 2-1 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Yanga ilimchezesha kwa mara ya kwanza beki wake mpya, Mbuyu Twite iliyemsajili kutoka APR ya Rwanda.
Twite alicheza nafasi ya kiungo mkabaji, ambayo aliimudu vyema kwa kuunganisha vizuri safu ya ulinzi iliyokuwa chini ya Kevin Yondan na Nadir Haroub 'Cannavaro' na ile ya ushambuliaji iliyokuwa ikiongozwa na Saidi Bahanunzi.
Pamoja na kufungwa, Coastal Union ilionyesha kandanda safi, hasa safu yake ya kiungo iliyokuwa ikiundwa na Jerry Santo, Razack Khalfan na Suleiman Selembe. Mshambuliaji Atupele Green alikuwa mwiba kwa mabeki wa Yanga.
Coastal Union ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Khalfan kwa kiki kali ya umbali wa mita 25 iliyotinga moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa Ally Mustapha 'Barthez' akiwa hana la kufanya. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Kutolewa kwa kadi nyekundu kwa Santo dakika za mwanzo za kipindi cha pili kwa kosa la kumtukana mwamuzi Hashim Abdalla baada ya kumpa kadi ya njano kwa kosa la kumchezea rafu Twite, kulipunguza makali ya Coastal Union.
Yanga ilisawazisha dakika ya 75 baada ya beki Philip Matusela wa Coastal Union kujifunga wakati akijaribu kuokoa krosi iliyopigwa na Shamte Ali kutoka winga ya kulia.
Zikiwa zimesalia dakika sita pambano hilo kumalizika, Bahanunzi aliiongezea Yanga bao la pili baada ya kugongeana vyena na Jerry Tegete.
No comments:
Post a Comment