'
Monday, May 17, 2010
FIFA ilianzishwa 1904 na nchi saba
SHIRIKISHO la Soka la Dunia (FIFA) lilianzishwa Mei 21 mwaka 1904 mjini Paris, Ufaransa. FIFA ilianzishwa kwenye makao makuu ya Muungano wa Vyama vya Michezo vya Ufaransa.
Makubaliano ya kuanzishwa kwa FIFA yalitiwa saini na wawakilishi wa viongozi wa vyama vya soka vya nchi saba. Vyama hivyo ni vya Ufaransa, Ubelgiji, Denmark, Uholanzi, Hispania, Sweden na Uswisi.
Mkutano mkuu wa kwanza wa FIFA ulifanyika siku mbili baadaye, Mei 23, 1904 na kumchagua Robert Guerin wa Ufaransa kuwa raia wake wa kwanza.
Victor Schneider wa Uswisi na Carl Anton Wilhelm Hirschmann wa Uholanzi walichaguliwa kuwa makamu wawili wa rais wakati Louis Muhlinghaus aliteuliwa kuwa katibu mku na mhasibu, akisaidiwa na Ludvig Sylow wa Denmark.
Viongozi hawa walikabiliwa na kazi ngumu kwa sababu FIFA haikuwa na fedha na wala muundo wa wanachama. Changamoto yao ya kwanza ilikuwa ni kubuni muundo mzuri, uundaji wa vyama vya soka vya kitaifa ili view wawakilishi wa uhakika na upatikanaji wa wanachama wapya.
Kazi ya kwanza ya uongozi huo ilikuwa kuishawishi Uingereza kwamba, uanachama wake katika shirikisho hilo ulikuwa wa muhimu. Uingereza ilikubali ombi hilo.
Katika miaka mitano ya kwanza, wanachama wa FIFA walitoka barani Ulaya pekee hadi mwaka 1909. Wanachama wa kwanza kutoka nje ya bara hilo walikuwa Afrika Kusini, Chile na Marekani.
Afrika Kusini ilijiunga na FIFA mwaka 1910, ikifuatiwa na Argentina na Chile zilizojiunga mwaka 1912. Marekani ilijiunga na shirikisho hilo mwaka 1913. Huu ulikuwa mwanzo wa FIFA kuwa na mtazamo wa kimataifa.
Kuzuka kwa vita ya kwanza ya dunia mwaka 1914 kulizusha tafrani kubwa miongoni mwa nchi wanachama. Hata hivyo, mahusiano ya kimataifa katika nchi hizo hayakuvunjika, japokuwa yaliendeshwa kwa tabu.
Jules Rimet alikuwa rais wa tatu wa FIFA mwaka 1921. Licha ya kuzuka kwa vita ya pili ya dunia chini yake, FIFA iliongeza wanachama wake na kufika 20. Wakati huo, Uingereza iliamua kujitoa FIFA. Katika kipindi chote hicho, si Brazil ama Uruguay iliyojiunge na FIFA.
Katika kipindi cha miaka 33 ya uongozi wake, Rimet aliweza kutimiza ndoto aliyokuwa nayo kwa miaka mingi ya kuanzisha fainali za Kombe la Dunia. Na wakati FIFA ilipoandaa fainali hizo kwa mara ya tano mwaka 1954 nchini Uswisi, wanachama wa shirikisho hilo waliongezeka na kufika 85.
Uamuzi wa FIFA wa kuandaa fainali za kombe la dunia ulifikiwa katika mkutano wake mkuu wa mwaka uliofanyika nchini Ufaransa mwaka 1928. Nchi zilizotuma maombi ya kuandaa fainali hizo zilizofanyika mwaka 1930, zilikuwa Hungary, Italia, Uholanzi, Hispania, Sweden na Uruguay.
Uruguay ndiyo iliyoteuliwa kuandaa fainali hizo kwa sababu moja muhimu. Nchi hiyo, ambayo ilitwaa ushindi wa jumla wa michezo ya Olimpiki mwaka 1924 na 1928, ilikuwa ikisherehekea kutimiza miaka 100 tangu kupata uhuru wake.
Fainali hizo zilianza Julai 18 mwaka 1930 kwenye uwanja wa Cenetary wa mjini Montevideo. Miaka minne baadaye, ‘Baba wa Kombe la Dunia’, Rimet alihitimisha ndoto yake ya muda mrefu baada ya fainali hizo kufanyika Ufaransa, nchi alikozaliwa.
Fainali za nne ilikuwa zifanyike mwaka 1942. Lakini uteuzi wa mwenyeji wa fainali hizo ulichelewa kutangazwa. Ulitangazwa mwaka 1938 katika mkutano uliofanyika mjini Paris. Zikaja kufanyika mwaka 1950 wakati Brazil ilipoteuliwa kuwa mwenyeji kutokana na kuwa nchi pekee iliyotuma maombi ya kuandaa fainali hizo.
Ungereza ilirejea FIFA mwaka 1946. Kulirejea kwa Uingereza kulitokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Rimet kwa kushirikiana na Arthur Drewry na Sir Stanley Rous.
Miaka minne baadaye, wakati wa fainali za kombe hilo zilizofanyika nchini Uswisi, Rimet wakati huo akiwa na umri wa miaka 80, aliamua kustaafu. Kwa mara ya mwisho, alikabidhi kombe la ubingwa wa dunia, wakati huo likijulikana kama ‘Kombe la Jules Rimet’ kwa nahodha wa Ujerumani.
Wakati wa uhai wake, Rimet aliteuliwa kuwa rais wa heshima wa FIFA kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa shirikisho hilo kabla ya kustaafu.
Rodolphe William Seeldrayers wa Ubelgiji alikuwa rais wa nne wa FIFA. Wakati wa uongozi wake, FIFA ilisherehekea kutimiza miaka 50. Wakati huo, idadi ya wanachama wake iliendelea kuongezeka na kufika 85.
Baada ya kuiongoza FIFA kwa miaka mitano na pia kuwa makamu wa rais chini ya Rimet kwa miaka 25, Seeldrayer alifariki dunia Oktoba mwaka 1955. Nafasi yake ilichukuliwa na Arthur Drewry, aliyechagulikuwa kuliongoza shirikisho hilo Juni mwaka 1956.
Kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, Arthur alikuwa mwenyekiti wa kamati iliyosimamia mabadiliko ya katiba na alikuwa msimamizi wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1958 zilizofanyika Stockholm, Sweden. Arthur alifariki dunia mwaka 1961 akiwa na umri wa miaka 70.
Kufuatia kifo hicho cha Arthur, shughuli za FIFA zilikuwa chini ya Ernst B Thommen wa Uswisi hadi Septemba 1961 wakati mkutano mkuu wa shirikisho hilo ulipomchagua Sir Stanley Rous kuwa rais wake wa sita. Thommen pia alikuwa msimamizi wa fainali za mwaka 1954, 1958 na 1962.
Chini ya uongozi wa Sir Stanley, idadi ya wanachama wa FIFA iliongezeka maradufu. Pia alianzisha utaratibu wa fainali hizo kuonyeshwa moja kwa moja kupitia kwenye televisheni katika nchi mbalimbali duniani.
Ikiwa kama taasisi binafsi, FIFA haikuwa ikipata misaada yoyote kutoka kwa serikali za nchi zilizo wanachama wake ama kutoka kwingineko. Mapato yake yalitokana na fainali za Kombe la Dunia.
Dk. Joao Havelange alichaguliwa kuwa rais wa saba wa FIFA mwaka 1974. Siku hiyo hiyo, Sir Stanley alitunukiwa hadhi ya kuwa rais wa heshima wa shirikisho hilo kutokana na mchango wake.
Dk. Havelange ndiye rais pekee wa FIFA aliyekaa madarakani kwa kipindi kirefu na kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa uendeshaji wa shirikisho hilo na pia muundo wake.
Kiongozi huyo anakumbukwa kutokana na jitihada zake kubwa zilizoliwezesha shirikisho hilo kuwa na mapato makubwa yatokanayo na fainali za Kombe la Dunia na pia kuwa na jengo lake la makao makuu lililopo mjini Zurich, Uswisi. Hivi sasa, FIFA ina wafanyakazi zaidi ya 120.
Dk.Havelange aliiongoza FIFA hadi Juni 8, 1998 na kumwachia kiti hicho rais wa sasa, Sepp Blatter wa Uswisi. Blatter ni rais wa nane wa FIFA.
Kabla ya uteuzi huo, Blatter aliitumikia FIFA kwa miaka 23, akiwa kwenye nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na katibu mkuu. Hivi sasa, FIFA inao wanachama 204.
Kwa sasa, uchaguzi mkuu wa FIFA unafanyika kila baada ya miaka minne na anachaguliwa na wajumbe kutoka nchi wanachama wa shirikisho hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment