KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 20, 2010

Hatuwezi kumzuia Yondani kwenda Yanga-Rage

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema hawawezi kumzuia beki wao nyota, Kelvin Yondani kujiunga na wapinzani wao wa jadi, Yanga.

Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Rage alisema timu yake inaundwa na wachezaji wengi wenye vipaji vya kucheza soka hivyo kuondoka kwa Yondani hakuwezi kuwa pigo kwao.

Rage alisema cha msingi kinachotakiwa kufanywa na mchezaji huyo ni kuheshimu na kufuata taratibu zote za usajili, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za kuaga kwa uongozi.

“Sina hakina kama ni kweli Yondani anataka kujiunga na Yanga, nimekuwa nikizisikia taarifa hizo kupitia kwenye vyombo vya habari, lakini kama ni za kweli, sisi hatuna kipingamizi chochote kwake,”alisema.

Ameutaka uongozi wa Yanga kufuata taratibu katika kumsajili mchezaji huyo kwa vile bado ana mkataba wa kuichezea Simba. Hakusema mkataba huo ni wa muda gani.

“Si busara hata kidogo kumzuia mchezaji kwenda kutafuta maslahi mazuri zaidi kwa sababu soka ndiyo kazi yake. Tunachosisitiza ni taratibu za usajili kufuatwa na kuheshimiwa,”aliongeza.

“Kama Yanga wamemuahidi mshahara mkubwa zaidi, ambao sisi hatuwezi kumpa, tupo tayari kumruhusu kwenda huko kwa moyo mweupe kabisa,” aliongeza.

Msimamo huo wa Simba umekuja siku chache baada ya vyombo vya habari kumnukuu Yondani hivi karibuni akisema kuwa, hivi sasa yupo huru baada ya mkataba wake na klabu hiyo kumalizika.

Vyombo hivyo vya habari vilimkariri Yondani akisema kuwa, atakuwa tayari kujiunga na Yanga iwapo klabu hiyo itampatia kitita cha sh. milioni 30.

Mbali na Yondani, imedaiwa pia kuwa, klabu ya Yanga inafanya mipango ya kumsajili mshambuliaji Emmanuel Okwi, aliyesajiliwa na Simba msimu uliopita akitokea Uganda.

No comments:

Post a Comment