KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Giggs: Hatupaswi kumtegemea Rooney pekee



LONDON, England

MSHAMBULIAJI mkongwe wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs amekiri kuwa, timu hiyo imeshindwa kutwaa taji la ligi kuu ya England msimu huu kwa sababu ya kumtegemea zaidi Wayne Rooney.

Giggs ni mchezaji anayeheshimika katika historia ya Manchester United, akiwa ameshinda mataji 11 ya ligi kuu ya England katika kipindi cha miongo miwili alichoichezea klabu hiyo, hivyo anapozungumza, watu humsikiliza.

Mshambuliaji huyo raia wa Wales alikiri kuwa, wachezaji wa Manchester United hawakutaka kutoka nje ya vyumba vya kubadili mavazi wakati wa mapumziko ya mechi yao dhidi ya Stoke City mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kubaini kuwa, Chelsea ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Wigan na kuelekea kutwaa ubingwa.

Lakini saa 24 baada ya Chelsea kutwaa taji hilo, Giggs alielezea kile kilichosababisha vijana wa Kocha Sir Alex Ferguson washindwe kung’ara msimu huu.

“Kama ulipaswa kusema kitu kimoja, pengine ungesema hatupaswi kumtegemea zaidi Rooney msimu ujao kama tulivyofanya msimu huu,”alisema Giggs.

“Tunahitaji kufunga mabao mengi zaidi kutoka maeneo tofauti na kutoka kwa wachezaji tofauti, japokuwa kama timu, tulifunga mabao mengi zaidi kuliko msimu uliopita,”aliongeza.

Giggs alisema safu ya ulinzi ya timu hiyo pia ilikuwa bora zaidi msimu huu kuliko msimu uliopita, lakini hawapaswi kumtegemea zaidi Rooney katika ufungaji mabao kama ilivyokuwa msimu huu.

Alisema katika mechi yao dhidi ya Stoke City, walianza kwa matumaini, lakini wakati wa mapumziko, walibaini kwamba Chelsea ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 na Wigan ilisaliwa na wachezaji 10 uwanjani.

“Tulielewa kwamba huo ulikuwa mwisho na kuwa wazi, hatukutaka kurejea uwanjani kwa ajili ya kipindi cha pili. Katika hali kama hiyo, unatamani kwenda nyumbani,”alisema.

Rooney ameifungia Manchester United mabao 34 msimu huu na kuumia kwake katika mechi ya awali ya robo fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani kuliashiria mwisho wa vijana hao wa Ferguson.

Baada ya hapo, Rooney hakuweza kufunga bao na Manchester United ikapoteza mwelekeo. Giggs anakiri kuwa, lilikuwa pigo kubwa kwa vijana wa Ferguson, ambao kamwe hawakuweza kuzinduka.

“Ilikuwa bahati nzuri kwetu kwamba Rooney aliumia katika kipindi muhimu cha msimu kwa sababu tungeendelea kutegemea magoli zaidi kutoka kwake na tusingeyapata,”alisema.

Giggs alisema hata kama kocha alisajili ama hakusajili washambuliaji wengine msimu huu, wachezaji walielewa kwamba walihitajika kufunga mabao zaidi.

“Hata kama mabeki walipanda mbele wakati wa kona au viungo walishambulia, sote tulihitajika kuchangia ushindi,”alisema.

Katika ligi ya msimu huu, Manchester United ilipata vipigo kutoka kwa Burnley, Aston Villa, Liverpool, Everton na Fulham, lakini Giggs amevitaja vipigo viwili kutoka kwa Chelsea kuwa ndivyo vilivyoamua mshindi wa ligi.

“Unaweza kusema tulipoteza mwelekeo kutokana na vipigo hivyo viwili kutoka kwa Chelsea. Kama tungetoka sare katika mchezo mmoja, tungeweza kutwaa ubingwa,”alisema.

Giggs alisema siku zote timu inapopoteza mechi mbili dhidi ya wapinzani wao wakubwa, hali inakuwa ngumu. Alisema siyo siku zote mechi hizo huamua mshindi, lakini ndivyo ilivyokuwa msimu huu.

“Na ukitazama ukweli kwamba Chelsea walitufunga sisi, Arsenal na Liverpool, nyumbani na ugenini, unapaswa kusema kuwa walistahili kutwaa ubingwa,”alisema.

Giggs alisema walivunjika nguvu kutokana na kupoteza baadhi ya pointi kwa sababu walipaswa kushinda mechi hizo na ingekuwa rahisi kwao kutwaa ubingwa msimu huu.

Pamoja na kuukosa ubingwa, Giggs alisema Manchester United inapaswa kupongezwa kwa vile imezidiwa kwa pointi moja na mabingwa wapya, Chelsea.

“Hakuna timu iliyoweza kufanya jambo hilo, hivyo wachezaji wanastahili pongezi kwa jitihada hizo. Lakini hivyo sivyo ilivyopaswa kuwa,”alisema.

Giggs (36), ambaye anatarajiwa kumaliza mkataba wa kuichezea Manchester United mwaka 2011, kabla ya kutundika daruga ukutani alisema, machungu ya kupoteza ubingwa msimu huu yataisaidia klabu hiyo katika mipango yake ya baadaye.

Alisema akiwa na umri wa miaka 17, walipoteza ubingwa kwa Leeds msimu wa 1991-92, tukio ambalo lilimwezesha kupata uzoefu na kuwa mchezaji wa kutumainiwa na Manchester United.

“Wachezaji hawa chipukizi, ambao hawaelewi lolote zaidi ya kushinda mataji katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, sasa watakabiliwa na changamoto niliyokutana nayo msimu wangu wa kwanza Manchester United,”alisema Giggs.

“Tulikaribia sana kutwaa ubingwa, lakini tuliupoteza kwa Leeds na hilo linakatisha tamaa kwa sababu, hisia za kushindwa kamwe hazitatoka kichwani mwako kwa msimu mzima,”aliongeza.

“Unapaswa kuhakikisha unakuja kwa nguvu na ukiwa mwenye kiu kubwa ya ubingwa msimu unaofuata, na hiyo ni alama ya timu bora na wachezaji wazuri,”alisema.

Giggs alisema kupoteza ubingwa kwa Leeds kulimsaidia kwa sababu hakutaka hisia hizo zimjie tena msimu uliofuata.

“Ushindi huleta hisia za ajabu, lakini hazidumu kwa muda mefu. Hisia za kufungwa zinadumu kwa muda mrefu na zinaumiza,”alisema.

Mshambuliaji huyo alisema ni rahisi kwa mchezaji kukabiliana na hisia za aina hiyo anapokuwa mtu mzima, lakini zinauma. Alisema mara nyingi wamekuwa wakijitahidi kuzisahau wanapokwenda mapumziko na familia zao.

Giggs alisema ana hakika kushindwa kwa timu yake kutwaa taji hilo msimu huu na kwa jinsi wachezaji walivyoonekana kukata tamaa, ana hakika watakuja na nguvu mpya msimu ujao.

“Kocha ametutaka tufurahie mapumziko yetu, iwe kwenye mapumziko maalumu ama kwenye fainali za Kombe la Dunia na kurejea msimu ujao tukiwa na nguvu mpya,”alisema.

“Tutakuwa tayari msimu ujao. Kocha ametutaka tukumbuke hisia za kupoteza ubingwa na kuhakikisha hatutarudia kosa hilo msimu ujao,”alisema.

No comments:

Post a Comment