KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, May 8, 2010

SERIKALI YAMSHANGAA WAMBURA

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeeleza kushangazwa na kitendo cha aliyekuwa mgombea uongozi katika uchaguzi mkuu wa Simba, Michael Wambura kufungua kesi mahakamani kupinga uchaguzi huo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera amesema kitendo hicho cha Wambura kimedhihirisha wazi kwamba si mwanamichezo kwa sababu masuala yanayohusu soka hayapaswi kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Bendera alisema inasikitisha kuona kuwa, wapo watu wanaofikisha masuala ya michezo mahakamani wakati zipo taratibu na vyombo maalumu vilivyowekwa kikatiba, vinavyopaswa kushughulikia mambo hayo.

Alisema katiba ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaeleza wazi kuwa, migogoro inayohusu soka haipaswi kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Naibu Waziri alisema migogoro ya michezo inapaswa kushughulikiwa na vyombo husika vilivyowekwa kikatiba na kila mwanamichezo anapaswa kuheshimu katiba ya chama ama klabu aliyomo.

Kauli hiyo ya Bendera imekuja siku chache baada ya Wambura kufungua kesi mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, akipinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Simba, uliopangwa kufanyika Jumapili ya Mei 9, 2010.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyofunguliwa na Wambura, mahakama ya Kisutu imetoa amri ya kusimamisha uchaguzi huo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Mbali na Wambura, mwanachama Juma Mtemi wa Simba naye amefungua kesi ya kupinga uchaguzi huo kwenye mahakama ya Ilala, ambayo juzi ilishindwa kutoa uamuzi kuhusu maombi yake kutokana na kufunguliwa kwa kesi nyingine kama hiyo kwenye mahakama ya Kisutu.

No comments:

Post a Comment