KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, May 8, 2010

KESI YA WAMBURA YATINGA MAHAKAMA KUU

Na Furaha Omary

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imeitisha mafaili ya kesi mbili za kupinga uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, zilizofunguliwa na wanachama Michael Wambura na Juma Mtemi.

Licha ya kuitishwa mafaili hayo kwa ajili ya kupitiwa upya, uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kisutu wa kusitisha kwa muda uchaguzi wa klabu hiyo, uliopangwa kufanyika Mei 9, unabaki palepale.

Msajili wa Mahakama hiyo, Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha alisema jana kuwa, kuitishwa kwa mafaili hayo, kumefanyika kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, Ismail Aden Rage na Hassan Othman 'Hassanoo'.

Alisema Mahakama Kuu iliamua kuitisha faili la kesi namba 100 ya mwaka 2010 iliyofuguliwa na Wambura dhidi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ili kupitiwa upya.

Mlacha alisema wamepata pia taarifa kwamba kuna kesi nyingine kama hiyo imefunguliwa mahakama ya Ilala na Mtemi dhidi ya kamati ya utendaji ya Simba, hivyo wameamua kuziunganisha.

Msajili alisema baada ya kuitishwa kwa mafaili hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo, Njengafibili Mwaikugile alielekeza wanaolalamika wapeleke malalamiko rasmi ya kisheria ili yasikilizwe na baada ya kuitwa pande zote mbili, ndipo Mahakama Kuu itoe maelekezo.

"Nilipompelekea Jaji Mfawidhi, ameipanga kwa Jaji Augustine Mwarija na kwa sababu muda wa saa kazi umekwisha, imeshindwa kusikilizwa, hivyo imepangwa Jumatatu,"alisema Mlacha.

Alisema jalada hilo litakapofika kwa Jaji Mwirija, ndipo atapanga muda wa wahusika kufika mahakamani na wa kusikilizwa.

Mapema wiki hii, Mahakama ya Kisuti ilisitisha kwa muda uchaguzi huo baada ya kukubali ombi lililowasilishwa na Wambura la kutaka kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo mpaka kesi yake ya msingi itakaposikilizwa.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Rita Tarimo baada ya upande wa mlalamikiwa, Hassan Dalali kutokuwa na pingamizi kuhusu ombi hilo.

Wakati huo huo, Rage amesema wamewasilisha malalamiko hayo Mahakama Kuu kuomba kupitiwa mafaili hayo kwa madai kuwa, utaratibu haukufuatwa wa kufunguliwa kwa kesi hizo.

No comments:

Post a Comment