Na Wilson Kimaro
HATMA ya uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba bado imeendelea kuwa kitendawili baada ya mahakama ya Ilala kupokea barua kutoka kwa mwanachama Juma Mtemi akidai kuwa, ameamua kuifuta kesi aliyofungua ya kupinga uchaguzi huo.
Hilo lilibainishwa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Janeth Kinyange wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo jana.
Hakimu Janeth alisema alipokea barua muda mfupi kabla ya kuingia mahakamani, ikiwa imeandikwa na Juma Mtemi ikitaka kesi hiyo ifutwe.
Alipoulizwa kupitia wakili wake, Jerome Msemwa, Mtemi alikana kuandika barua hiyo na kusema hata sahihi iliyokuwemo haikuwa yakwake bali ilighushiwa.
Wakili Jerome aliiomba nakala ya barua hiyo kwa lengo la kufungua kesi ya jinai ya kughushiwa kwa jina na saini ya mteja wake.
Kabla ya kuzuka kwa utata wa barua hiyo, Hakimu Janet aliamua kuiahirisha kesi hiyo hadi leo na kuutaka uongozi wa Simba ukubaliane juu ya nani wakili wao.
Hakimu Janeth alifikia uamuzi huo baada ya Wakili, Peter Swai kuwasilisha barua mahakamani hapo iliyotiwa saini na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Omari Gumbo ikimtambua kuwa ndiye wakili wa utetezi.
Mbali na barua hiyo, mahakama pia ilipokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ikitoa taarifa kuwa Wakili Majura Magafu ndiye anayeiwakilisha klabu hiyo.
Kufuatia utata huo, Hakimu Janeth alisema mahakama ipo njia panda juu ya wakili gani anayepaswa kuiwakilisha klabu hiyo.
Aliutaka ungozi wa Simba kukutana na kujadili kwa kina kabla ya kuamua juu ya mwakilishi wao mahakamani na kusisitiza kwamba kazi ya mahakama ni kutoa uamuzi juu ya suala hilo.
Kesi hiyo ya madai ilifunguliwa na Mtemi mwanzoni mwa wiki hii akipinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Simba.
Mtemi alifungua kesi hiyo siku chache baada ya Michael Wambura kuenguliwa kugombea nafasi ya mwenyekiti na kueleza azma yake ya kufungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo.
Wambura alienguliwa kugombea wadhifa huo na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatia rufani iliyowasilishwa na mwanachama Daniel Kamna.
No comments:
Post a Comment