Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam imesimamisha kwa muda uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba uliopangwa kufanyika Jumapili ya Mei 9, 2010.
Uamuzi huo wa mahakama umekuja, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Michael Wambura, ambaye amefungua kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.
Katika madai yake, Wambura anataka haki itendeke baada ya kuenguliwa kuwania uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Katika kuomba haki, Wambura pia ameitaka mahakama imlinde asije kuchukuliwa hatua zozote za kufikishwa mahakamani hadi shauri lake kuu litakapoamuliwa.
Kwa mujibu wa katiba ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ni marufuku kwa masuala yanayohusu soka kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
Hati ya kusimamisha uchaguzi huo, imetolewa na Hakimu Tarimo wa Kisutu. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Mei 31 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment