KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 17, 2010

Kombe la Dunia lilianzishwa na Jules Rimet





HAKUNA michuano mingine yenye msisimko na inayovuta watu wengi duniani kama fainali za soka za Kombe la Dunia, zinazoandaliwa kila baada ya miaka minne na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

Tangu fainali hizo zilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1930 nchini Uruguay,, FIFA imezidi kukua, kupata umaarufu na mafanikio makubwa kutokana na mchezo wa soka.

Wazo la kuandishwa kwa fainali za Kombe la Dunia lilianza nchini Ufaransa mwaka 1920 kutoka kundi moja la Wafaransa, likiongozwa na Jules Rimet.

Kombe la kwanza la dunia lililotengenezwa kwa kutumia madini ya dhahabu, lililopewa jina la Jules Rimet, lilishindaniwa mara tatu miaka ya 1930 kabla ya vita ya pili ya dunia, iliyosababisha fainali hizo zisifanyike kwa miaka 12.

Fainali hizo ziliporejea tena mwaka 1950, zilizidi kupata umaarufu mkubwa na kuwa pekee zenye msisimko na mvuto duniani.

Ziliingia doa mwaka 1966 baada ya kombe la awali la dunia kutoweka katika mazingira ya kutatanisha nchini England, lakini baadaye liligunduliwa likiwa limezikwa ardhini chini ya mti na mbwa mdogo, aliyekuwa akiitwa Pickles.

Kombe hilo lilitoweka tena mwaka 1983 baada ya kuibwa na wezi, safari hii mjini Rio de Janeiro na baadaye kuyeyushwa. Shirikisho la Soka la Brazil, ambalo lilipewa haki ya kulitunza kombe hilo, kufuatia timu ya taifa ya nchi hiyo kulitwaa mara tatu, liliamua kutengeneza kombe lingine.

Kombe la mwanza la dunia lilikuwa na urefu wa sentimita 3.8. Kombe hilo lilitengenezwa kwa kutumia mchanganyiko wa madini ya fedha na dhahabu na jiwe la ‘semi-precious’.

Kati ya mwaka 1930 na 1970, kombe hilo liliwekwa sahani ya dhahabu katika pande zote nne za chini, ambako yaliandikwa majina ya nchi zilizowahi kulitwaa.

Tangu kuanzishwa kwake, fainali hizo zilikuwa zikifanyika katika nchi moja za Ulaya na Amerika hadi mwaka 1996 wakati Kamati ya Utendaji ya FIFA ilipoziteua Japan na Korea Kusini kuandaa fainali hizo kwa pamoja mwaka 2002 na kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Kwa kipindi cha miaka 16 tangu fainali hizo zilipoanzishwa mwaka 1930, nchi saba zimetwaa ubingwa wa dunia. Nchi hizo ni Uruguay, Italia, Ujerumani, Brazil, England, Argentina na Ufaransa.

Brazil ndiyo inayoongoza kwa kutwaa ubingwa mara tano kuanzia mwaka 1958, 1962, 1970, 1994 na 2002. Inafuatiwa na Italia, iliyotwaa ubingwa mara nne, kuanzia mwaka 1934, 1938, 1982 na 2006.

Ujerumani imetwaa kombe hilo mara tatu, mwaka 1954, 1974 na 1990 wakati Uruguay imelitwaa mara mbili, 1930 na 1950 sawa na Argentina, iliyolitwaa 1978 na 1986 England na Ufaransa zimetwaa kombe hilo mara moja kila moja, 1966 na 1998.

Awali, nchi nyingi kutoka Ulaya na Amerika ya Kusini ndizo zilizokuwa zikishiriki kwenye fainali hizo. Lakini kukua kwa soka katika kanda zingine za Ulaya, Asia na CONCACAF kuliifanya FIFA iongeze idadi ya timu kutoka kanda hizo.

Maajabu yaliyoifanya FIFA ikubali kuongeza idadi ya timu ni pamoja na kipigo ilichokipata England kutoka kwa Marekani mwaka 1950, kipigo ilichokipata Italia kutoka kwa Korea Kusini mwaka 1966 na kufuzu kwa Cameroon kucheza robo fainali mwaka 1990.

Hivi sasa, fainali za Kombe la Dunia zimekuwa zikitazamwa na watu wengi duniani kupitia kwenye televisheni. Kwa mfano, inakadiriwa kuwa, watu bilioni 37 walitazama fainali za mwaka 1998 zilizofanyika Ufaransa, ikiwa ni pamoja na watu bilioni 1.3 waliotazama mechi ya fainali pekee wakati zaidi ya watu milioni 2.7 walifika kwenye viwanja mbalimbali kutazama mechi 64 zilizochezwa mwaka huo kwenye viwanja vya Ufaransa.

Hata hivyo, baada ya miaka yote hiyo na mabadiliko mengine, mwelekeo wa fainali hizo umebaki kuwa ni ule ule wa timu zinazoshiriki kuwania kombe la dunia, lililotengenezwa kwa madini ya dhahabu.

No comments:

Post a Comment