KIKOSI cha timu ya soka ya Simba kinatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Rwanda kushiriki katika michuano ya Kombe la Kagame huku wachezaji Emmanuel Okwi na David Naftali wakiachwa katika safari hiyo.
Mbali ya wachezaji hao kuachwa, timu hiyo inakabiliwa na majeruhi wawili, ambao ni washambuliaji Uhuru Selemani na Ramadhani Chombo.
Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri alisema, licha ya kuwa majeruhi, Uhuru na Chombo wataambatana na timu hiyo nchini Rwanda.
Phiri alisema timu yake imeajiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo licha ya kupangwa kwenye kundi gumu. Simba imepangwa kundi moja na timu za Sofapaka ya Kenya, URA ya Uganda na Atraco ya Rwanda.
Kocha huyo raia wa Zambia alisema, kikosi chake kinakwenda kwenye mashindano hayo kikiwa na dhamira ya kupigana kufa au kupona ili kitwae ushindi.
Phiri alikiri ushiriki wa timu yake katika mashindano ya Kombe la Shirikisho, umeipa maandalizi mazuri kwa ajili ya michuano hiyo, inayotarajiwa kuanza keshokutwa, ikizishirikisha timu bingwa kutoka nchi za mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
"Kwa kweli tumejipanga vizuri na tunatarajia kufanya vizuri katika mashindano hayo, japokuwa mwaka huu yatakuwa magumu kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita," alisema Phiri.
Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholaus Musonye, alisema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mashindano hayo yamekamilika.
Musonye alisema timu shiriki zimeshaanza kuwasili nchini Rwanda kwa ajili ya mashindano hayo, zikiwemo timu za Heart Land ya Nigeria na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambazo zitakuwa waalikwa.
Timu zingine zinazotarajiwa kushiriki michuano hiyo, nchi zinazotoka zikiwa kwenye mabano ni Sofapaka (Kenya), Mafunzo (Zanzibar), URA (Uganda), Vital’ O (Burundi), St. George (Ethiopia), Telecom (Somalia), Atraco na APR za Rwanda.
No comments:
Post a Comment