KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

Drogba amtamani Torres


Drogba

LONDON, England

MSHAMBULIAJI Didier Drogba wa Chelsea amesema anamkaribisha kwa mikono miwili Fernando Torres wa Liverpool iwapo atasajiliwa na klabu yake.

Kauli hiyo ya Drogba imekuja siku chache baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Chelsea imetenga pauni milioni 70 za Uingereza (sh. bilioni 140) kwa ajili ya kumsajili Torres.

Gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti wiki iliyopita kuwa, mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich amepania kuvunja rekodi ya uhamisho wa wachezaji katika ligi kuu ya England kwa kusajili kifaa kipya kwa bei kali.

Kwa sasa, rekodi hiyo inashikiliwa na beki Rio Ferdinand, aliyesajiliwa na Manchester United kwa uhamisho wa pauni milioni 29.1 kutoka klabu ya Leeds miaka minane iliyopita.

Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay alithibitisha mapema wiki hii kuwa, Kocha Carlo Ancelotti atapatiwa fedha anazotaka ili kusajili mchezaji mmoja au wawili na kwamba lengo lao kubwa ni kumnasa Torres.

Akizungumza mjini hapa juzi usiku, Drogba alisema atakuwa na furaha kubwa iwapo Torres ataungana naye katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea.

Alisema kujiunga kwa Torres kutaifanya safu ya ushambuliaji ya Chelsea iwe tishio kwa mabeki wa klabu za timu pinzani kokote duniani.

“Bila shaka nitamkaribisha Torres kwa mikono miwili,”alisema Drogba, ambaye ameibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya England baada ya kupachika wavuni mabao 36 msimu huu.

“Kila wakati mchezaji mpya anakuja hapa, hilo linaifanya klabu iwe kubwa zaidi na kutuongezea nguvu,” alisema Drogba.

“Kama kuna nafasi ya yeye kuja hapa, anakaribishwa kwa sababu msaada wowote unahitajika,”aliongeza.

Mbali na Chelsea, klabu nyingine iliyoonyesha dhamira ya kumsajili Torres ni Manchester City, ambayo ipo tayari kutoa dau lolote ili kumnasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Hispania.

Torres (26) ameonyesha nia ya kutaka kuihama Liverpool baada ya kushindwa kutwaa taji lolote tangu alipojiunga na klabu hiyo miaka mitatu iliyopita.

No comments:

Post a Comment