KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

TENGA: RAGE NI MPIGANAJI

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limempongeza Mwenyekiti mpya wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kwa kumuelezea kuwa ni mpiganaji halisi katika masuala yanayohusu michezo.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Rage ni mmoja wa wadau, ambaye amepigana kwa hali na mali kulinda na kutetea katiba ya Simba, TFF na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

“Kwa kweli nawapongeza wadau wa klabu ya Simba na hasa Rage, aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti,”alisema Tenga.

Alisema kimsingi katiba zote zinapinga kitendo cha mgombea kupeleka suala la michezo kwenye mahakama za kawaida na kusisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kosa kikatiba.

Tenga alisema inapotokea migogoro ya aina hiyo, muhusika anapaswa kufuata taratibu zilizowekwa kikatiba katika kutafuta haki yake badala ya kukimbilia mahakamani.

"Tayari soka yetu imekuwa ikikua kila kukicha na tulishaanza kusahau masuala ya watu kwenda mahakamani, lakini nashakuru kwa wadau ambao wameongozwa na Rage kuhakikisha wamesimamia matakwa ya katiba na uchaguzi umefanyika kama ilivyopangwa," alisema.

Rais huyo wa TFF alisema kitendo cha baadhi ya wanachama wa Simba kwenda mahakamani kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo, kungeiweka Simba kwenye hatari ya kufungiwa na FIFA.

Alisema kufanyika kwa uchaguzi wa Simba, siyo mafanikio pekee ya klabu hiyo bali soka ya Tanzania kwa ujumla.

"Maamuzi ya kufanyika kwa uchahuzi wa Simba yalitolewa usiku wa Ijumaa iliyopita, binafsi sikutarajia wanachama 1,500 wangejitokeza kwenda kupiga kura," alisema.

Ametoa wito kwa wanachama wa klabu zingine, kuiga mfano wa Simba na kuchagua viongozi wenye uwezo mkubwa wa kutafsiri na kutekeleza katiba zao kama alivyofanya Rage.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita, Rage alichaguliwa kuwa mwenyekiti baada ya kumshinda Hassan Othman Hassanoo. Uchaguzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment