KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 12, 2011

Nature, Chege, Temba wakutanishwa kwenye filamu

Chege

Juma Nature

Temba


KATIKA hali, ambayo haikutarajiwa na mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya, wasanii wanaounda makundi mawili ya TMK Wanaume Family na TMK Wanaume Halisi wanatarajiwa kucheza filamu ya pamoja.
Filamu hiyo, inatarajiwa kuongozwa na mtaalamu wa studio wa TMK Wanaume, Hassan Umande, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Chichi.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Chichi alisema, maandalizi kwa ajili ya filamu hiyo yanaendelea vizuri.
Chichi alisema kwa sasa wanakamilisha kuandaa mwongozo wa filamu hiyo, utakaochukua wiki mbili kukamilika.
Baadhi ya wasanii nyota wa makundi hayo, wanaotarajiwa kucheza filamu hiyo ni pamoja na Juma Nature, Chege Chigunda, Mheshimiwa Tembe na Rashid Ziada ‘KR’.
Kwa mujibu wa Chichi, lengo la kuandaa filamu hiyo ni kuelezea historia ya wanamuziki wa kundi hilo, walikoanzia safari yao ya muziki hadi kufika walipo sasa.
Chichi alisema wasanii wa makundi yote mawili watashiriki kucheza filamu hiyo bila kubagua wenye majina makubwa na wale chipukizi.
Mbali na kuandaa mwongozo, Chichi alisema wameshaanza kazi ya kuunganisha nyimbo zilizorekodiwa awali na studio hiyo, ambazo zitaingizwa kwenye filamu hiyo.
Kutokana na gharama za kutengeneza filamu hiyo kuwa kubwa, Chichi amewataka wadhamini mbalimbali kujitokeza kuidhamini ili iweze kukamilika mapema.
Wasanii wa makundi hayo mawili, zamani walikuwa wakiunda kundi moja la TMK Wanaume Family na kufanyakazi chini ya meneja wao, Saidi Fela.
Baadaye, Juma Nature na baadhi ya wasani wenzake, waliamua kujitenga na kuanzisha kundi lao la TMK Wanaume Halisi. Fela bado anaendelea kuongoza kundi la TMK Wanaume Family.

No comments:

Post a Comment