KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 5, 2011

Daktari wa Yanga atupwa 'lupango'

KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia mechi tatu za ligi hiyo daktari wa timu ya Yanga, Juma Sufiani kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa, uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika juzi mjini Dar es Salaam.
Wambura alisema, Sufiani amefungiwa kwa kosa la kumsukuma mchezaji mmoja wa Azam wakati wa mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya timu hizo, iliyochezwa Machi 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Wambura, daktari huyo wa Yanga ataanza kutumikia adhabu hiyo kuanzia msimu ujao wa ligi. Katika mechi hiyo, Sufiani alitolewa kwenye benchi la wachezaji wa akiba kwa kosa hilo.
Ofisa Habari huyo wa TFF alisema, suala la mchezaji Mohamed Hussein na Gaudence Mwaikimba wa Kagera Sugar limepelekwa kwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya hatua zaidi.
Mohamed anatuhumiwa kumtukana mwamuzi msaidizi, Saada Hussein wakati wa mechi kati ya timu hiyo na AFC, iliyochezwa Aprili 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Naye Mwaikimba anatuhumiwa kuwafuata vyumbani na kuwatukana waamuzi waliochezesha mechi hiyo mara baada ya pambano hilo kumalizika.
Wambura alisema, kwa mujibu wa kanuni, makosa yote ya kinidhamu yanayotokea nje ya uwanja, adhabu zake zinatolewa na Kamati ya Nidhamu, ambayo kwa sasa inaongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) mstaafu, Alfred Tibaigana.

No comments:

Post a Comment