KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 5, 2011

GENEVIEVE NNAJI: Nitafunga ndoa baada ya kumpata mwanaume bora


LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa Nigeria, Genevieve Nnaji amesema, atafunga ndoa baada ya kumpata mwanaume anayeamini atakuwa sahihi katika maisha yake.
Genevieve alisema hayo wiki hii alipokuwa akihojiwa na gazeti la Encomium la Nigeria. Gazeti hilo ndilo lililomzawadia tuzo ya mwanamke mwenye mvuto zaidi nchini humo.
“Bado namtafuta mwanamke sasa na kama nitampata, nitafunga ndoa. Ukweli unabaki palepale kwamba sitafuti wanaume. Nakiri kwamba wanavutiwa na kazi yangu,”alisema mwanadada huyo.
“Lakini sio wanaume pekee, wapo wanawake, ambao pia wanavutiwa na kazi yangu. Sitafuti wanaume na pia sifikirii iwapo wapo wanaume wanaonitafuta,”aliongeza.
Mwanadada huyo alisema anaona fahari kubwa kwa kushinda tuzo ya mwanamke mwenye mvuto zaidi nchini Nigeria na kuongeza kuwa hiyo ni heshima kubwa kwake.
Genevieve (30) alikanusha madai kuwa, amekuwa akijihusisha na usagaji kwa wanawake wenzake, ndio sababu hana mwanaume.
Alisema kamwe katika maisha yake hatarajii kujihusisha na tabia hiyo na haelewi kwa nini baadhi ya watu na vyombo vya habari wamekuwa vikivumisha habari hizo.
“Mimi si msagaji, na mbali na hilo, sijawahi kusema nina uhusiano na mwanamke yeyote, siwezi kufanya hivyo katika maisha yangu,”alisisitiza.
Alipoulizwa ni aina gani ya mwanaume, ambaye angependa kufunga naye ndoa katika maisha yake, Genevieve alisema atafahamu hilo baada ya kukutana na mwanaume huyo.
Genevieve hakuwa tayari kukubali ama kukataa kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki nyota wa nchi hiyo, D’Banj kwa sababu suala hilo linahusu maisha yake binafsi.
“Sipenzi kuzungumza kuhusu maisha yangu binafsi, iwe ni kweli ama uongo. Ni suala linalohusu maisha yangu binafsi. Ni jambo linalonihusu mimi binafsi,”alisema.
Mcheza filamu huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto alisema, katika maisha yake, ana uwezo wa kukutana na mwanaume yeyote anayempenda.
Akizungumzia maisha yake kimuziki, Genevieve alisema hatarajii kuendelea tena na fani hiyo kwa sababu aliamua kujihusisha nayo kwa muda mfupi.
Alisema muziki kwake ilikuwa ni kazi ya mpito na kwamba ilitokana na mkataba alioupata kwa ajili ya kurekodi baadhi ya nyimbo.
“Sijaachana kabisa na muziki. Pia sijaamua kuufanya muziki uwe kazi yangu ya kudumu. Kuwa mkweli, sielewi iwapo nitaendelea kujihusisha na fani ya muziki,”alisema.
Mwanadada huyo alikiri kuwa, amepata mafanikio makubwa katika kazi ya uigizaji filamu kwa vile anaipenda na kuifanya kwa moyo wake wote.
Genevieve alisema kwa sasa hatarajii kujihusisha na utayarishaji wa filamu zake kama ilivyo kwa waigizaji wenzake. Alisema kwa sasa bado anapenda kuendelea kucheza sinema.
Mrembo huyo pia alikanusha madai kuwa, hana uhusiano mzuri na mwigizaji mwenzake nyota nchini humo, Omotola Jalade. Alisema yeye na Omotola ni marafiki wa muda mrefu na wameshiriki kucheza filamu nyingi pamoja.
“Nafikiri nimecheza filamu nyingi zaidi na Omotola kuliko waigizaji wengine wote wa kike. Tumeigiza kama ndugu kwenye filamu nyingi,”alisema.
“Inachekesha kwa sababu hatukupaswa kuwa marafiki nab ado tunafanyakazi pamoja, lakini nataka watu waelewe kuwa hatuna ugomvi wowote,”aliongeza.
Genevieve alisema anaamini taarifa hizo zimekuwa zikivumishwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa malengo yao binafsi, hasa biashara, lakini bado wao wataendelea kuwa marafiki.
Mcheza filamu huyo anavutiwa zaidi na filamu yake, inayojulikana kwa jina la Crash. Anapendelea zaidi kula wali. Anavutiwa na pafyumu ya Coco Chanel.
Msemo unaomvutia zaidi ni ule unaosema: “Wafanyie wenzako kile ambacho wewe unataka wakufanyie.”

No comments:

Post a Comment