KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, April 8, 2011

JULIO: Kuitoa Cameroon inawezekana


TIMU ya soka ya taifa ya vijana wa chini ya miaka 23 ya Tanzania, Vijana Stars, mwishoni mwa wiki iliyopita ilichapwa mabao 2-1 na Cameroon katika mechi ya awali ya raundi ya kwanza ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2013. Katika makala hii, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu anaelezea nafasi ya timu hiyo katika mechi ya marudiano, itakayochezwa keshokutwa mjini Dar es Salaam.

SWALI: Unadhani ni kitu gani kilichosababisha timu yako ifungwe katika mechi yenu ya awali iliyochezwa nchini Cameroon?

JIBU: Kikosi changu kilicheza vizuri, ingawa kulitokea tatizo dogo ambalo lilisababisha kufungwa. Kwa jumla nawapongeza wachezaji wangu kwa kuonyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo. Wapinzani wetu sio wabaya. Ni timu nzuri na inaundwa na wachezaji wengi wanaocheza soka ya kulipwa Ulaya na ndio walioisaidia kwa kiasi kikubwa katika mechi hiyo. Hata hivyo, nafasi ya kusonga mbele kwetu bado ni kubwa. Bado vijana wangu wana ari kubwa ya kushinda mechi ya marudiano. Ili hilo liwezekane, nimeamua kubadili mfumo wa mazoezi. Nimeamua kuwapeleka gym wachezaji wangu kwa lengo la kuwaongezea nguvu za mwili na stamina ili waweze kukabiliana vyema na wapinzani wetu, ambao wanacheza mpira wa kutumia nguvu zaidi kuliko akili. Mbali na mazoezi hayo, nimekuwa nikiwapa pia mafunzo ya darasani ili kuhakikisha wanauelewa vyema mfumo ninaowafundisha wa kulinda na kushambulia.

SWALI: Unadhani mafunzo hayo yatawawezesha vijana wako kushinda mchezo wa Jumamosi? JIBU: Mimi pamoja na benchi langu la ufundi tuna imani kubwa kwamba vijana wanayaelewa na kuyazingatia vyema mafunzo tunayowapatia na wana uwezo wa kuishinda Cameroon. Kama nilivyosema awali, Cameroon hawatishi sana kama tulivyokuwa tukiwafikiria. Lazima tuwafunge katika mechi ya Jumamosi. Hilo lipo wazi kwa sababu tunajivunia kwamba tutakuwa tukicheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani.

SWALI: Huoni kama kuna tatizo kwenye kikosi chako kutokana na baadhi ya wachezaji muda mwingi kuwa katika timu zao, kama Mbwana Samatta na wengineo wanaocheza ligi kuu?

JIBU: Kuchelewa kujiunga kambini kwa baadhi ya wachezaji kunaweza kukasababisha kuwepo kwa baadhi ya mapungufu katika mfumo wa uchezaji, lakini bado hilo sio tatizo kubwa sana. Kwa vile wanaelewana wanapokuwa uwanjani, nadhani hakutakuwa na matatizo makubwa.

SWALI: Je, umekuwa ukipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika maandalizi ya mchezo huo?

JIBU: Kwa kweli nawashukuru sana viongozi wa TFF kwa vile wamekuwa karibu sana na sisi katika maandalizi ya kuhakikisha timu yetu inaifunga Cameroon. Pia napenda kuwapongeza viongozi wa serikali kutokana na kutuunga mkono na mara kadhaa wamekuwa wanakuja kuangalia jinsi tunavyoendelea na maandalizi ya kuiua Cameroon.

SWALI: Una ujumbe gani kwa mashabiki wa soka hapa nchini kuhusu mchezo wa Jumamosi ama unatoa ahadi gani?

JIBU: Nawaomba mashabiki wa soka, bila kujali itikadi zao, wafike kwa wingi kwenye uwanja wa Taifa na kuwashangilia kwa nguvu zote wachezaji wetu ili tuweze kushinda mchezo huo. Ieleweke kuwa, ushirikiano wa mashabiki ni jambo muhimu katika kupata ushindi. Wachezaji wanayo sehemu yao, lakini sehemu nyingine muhimu ya ushindi hutokana na mashabiki. Tunahitaji bao moja pekee ili kusonga mbele na hilo linawezekana.

SWALI: Timu yako imeweka kambi wapi na kuna matatizo yoyote yaliyojitokeza kambini hadi sasa?

JIBU: Tumeweka kambi Mbamba Beach na namshukuru Mungu kwamba hadi sasa hakuna tatizo lolote lililojitokeza. Kambi ipo katika mazingira mazuri na wachezaji wanaifurahia. Deni tulilonalo kwa watanzania ni kushinda mechi hiyo muhimu.

SWALI: Kutakuwepo na mabadiliko yoyote kwenye kikosi chako kitakachocheza Jumamosi na kile kilichocheza Cameroon?

JIBU: Sidhani kama kutakuwepo na mabadiliko makubwa. Hiyo inategemea na hali za wachezaji zitakavyokuwa. Bado ninaendelea na mazoezi ya kuangalia nani atakuwa fiti zaidi kwa ajili ya mchezo huo. Upangaji wa timu pia utategemea na mfumo tunaotumia. Ni mapema mno kutaja kikosi kitakachocheza mechi hiyo kwa sasa.

No comments:

Post a Comment