KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 28, 2011

JKT yamwekea ngumu Kazimoto



KLABU ya Simba iko katika hati hati ya kumpata kiungo Mwinyi Kazimoto wa JKT Ruvu baada ya kigogo wa timu hiyo kuwa mbogo.
Mwenyekiti wa JKT Ruvu, timu inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa nchini, Charles Mruge juzi alikaririwa na Radio Uhuru akisema ni vigumu kwa Kazimoto kwenda Simba.
Kiongozi huyo alisema, mchezaji wake hawezi kuchezea Simba kwa sababu ni mwajiriwa wa jeshi hilo na anapaswa kufuata taratibu za kuacha kazi kwanza kabla ya kutangaza anahama timu.
“Kazimoto ni mwajiriwa wa jeshi, sijui kwa nini Simba wanatangaza wamemsajili wakati wanafahamu hawezi kuchezea timu za uraia,” alisema mwenyekiti huyo.
Alisema juzi alikuwa Zanzibar kikazi na alitarajia kurejea Dar es Salaam, ambapo amepanga kuzungumza na Kazimoto binafsi kujua msimamo wake kabla ya kutoa taarifa yoyote kuhusu sakata hilo.
“Sina taarifa za kutoka Simba kuhusu huyu mchezaji ila nimesoma katika magazeti kuwa anakwenda Simba, kwa sasa siwezi kuzungumza zaidi mpaka nikutane na mchezaji mwenyewe,” alisema Mruge.
Kazimoto inaaminika ni miongoni mwa viungo bora nchini, ambaye klabu ya Simba imemtupia ndoano, ambapo ili ifanikiwe kumpata, inalazimika kumtoa kwenye ajira.
Hata hivyo, mara kadhaa wachezaji wanaocheza katika timu za jeshi wamekuwa na wakati mgumu kuhama kipindi cha usajili kinapofika, ambapo baadhi ya wanasoka waliowahi kupata kasheshe ni Primus Kasonzo na Heri Morris, ambao walikuwa katika timu ya Tanzania Prisons ya Mbeya.

No comments:

Post a Comment