KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 3, 2011

MAPACHA WATATU: Tumekamilika kila idara


BENDI ya muziki wa dansi ya Mapacha Watatu imejigamba kuwa, kwa sasa imekamilika katika kila idara baada ya kuajiri wanamuziki wapya zaidi ya sita.
Wakizungumza mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, wakurugenzi wa bendi hiyo, Jose Mara, Khalid Chokoraa na Kalala Junior walisema, wamepania kufunika soko la muziki nchini.
Kwa mujibu wa Jose, wanamuziki wapya walioajiriwa na bendi hiyo ni wapiga magita ya solo, besi, rythim, drums, tumba na wacheza shoo wanne.
Jose alisema katika safu ya uimbaji, wameamua kuajiri wanamuziki wasiokuwa na majina kwa lengo la kuibua vipaji vyao na kuwaendeleza.
“Tulipoanzisha bendi yetu tulikuwa waimbaji watatu, lakini sasa tumeongeza wengine watatu. Hatutaki waimbaji wenye majina makubwa kwa sababu ya kuepuka matatizo,”alisema.
“Unajua wapo vijana wengi wenye vipaji na uwezo wa kuimba, lakini hawajulikani. Mimi nilionekana mtaani, mtu mmoja akaenda kuwaambia FM Academia kuna kijana tukimpata atatufaa sana, hivyo na sisi tumefuata nyayo hizo kwa kuajiri wanamuziki wasiokuwa na majina,”aliongeza.
Kwa upande wake, Kalala alisema wamepata msaada mkubwa wa kuanzisha bendi hiyo kutoka kwa baba yake, Komandoo Hamza Kalala na mpuliza saxaphone maarufu nchini, Mafumu Bilali ‘Bombenga’.
Kalala alisema binafsi haoni umuhimu wa kujiunga na familia yake kuanzisha bendi yao kama ilivyo kwa familia zingine, lakini alidokeza kuwa, wanajiandaa kurekodi albamu ya familia.
Mbali na Kalala Junior, mtoto mwingine wa familia ya mwanamuziki huyo mkongwe nchini ni Totoo Kalala, ambaye ni repa wa bendi ya FM Academia.
Naye Chokoraa alisema, kwa sasa wanajiandaa kuipua albamu yao ya pili na tayari wamesharekodi nyimbo tano. Alisema nyimbo iliyosalia inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.
Alipoulizwa kuhusu tetesi kwamba, yeye na Kalala huenda wakarejea tena katika bendi yao ya zamani ya Twanga Pepeta International, Chokoraa alisema uvumi huo hauna ukweli wowote.
“Sisi sote hapa unapotuona ni wakurugenzi, hivyo hatuwezi kutoka kwenye bendi tuliyoianzisha wenyewe,”alisema.
“Tunachoweza tu kusema ni kwamba bendi yetu imekamilika katika kila idara kwa sababu tunao wapiga ala mbalimbali, waimbaji wengine watatu na wacheza shoo,”alisema.
Kwa mujibu wa Jose, bendi yao imesajiliwa kwa jina la Mapacha Watatu na hawawezi kubadili jina hilo kwa sababu hiyo ni nembo ya utambulisho wao.
“Jina hili halina maana kwamba sisi ni watoto mapacha. Hata Lady JayDee anayo bendi inaitwa Machozi, hii haina maana kwamba wanapokuwa wakiimba jukwaani, huwa wanalia,”alisema Jose.
Alisisitiza kuwa, bendi yao kamwe haiwezi kufa hata kama itatokea mwanamuziki mmoja ameamua kujiengua na kujiunga na bendi nyingine.
“Mapacha Watatu ni kama Wenge Musica BSBG, haiwezi kufa. Wenge wameondoka wanamuziki wengi, lakini bendi ipo palepale,”alisisitiza.
Amewashukuru mashabiki wa muziki nchini kwa kuwapa moyo, kuwaunga mkono na kujitokeza kwa wingi kuhudhuria maonyesho yao. Alisema wanapata faraja kubwa na kuahidi kukonga nyoyo zao zaidi kwa kuwaandalia burudani murua.
Kwa mara ya kwanza, wimbo wa ‘Shika nikushike’ wa bendi hiyo umeingizwa katika tuzo za muziki za Kilimanjato za mwaka 2010 zinazotarajiwa kutolewa hivi karibuni.
Wimbo huo umeshindanishwa katika kundi la wimbo bora wa Kiswahili wa bendi pamoja na nyimbo za Laptop wa Extra Bongo, Laptop wa Twanga Pepeta na Pongezi kwa wanandoa wa Akudo Impact.


No comments:

Post a Comment