KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 24, 2011

Ochan, Okwi wamlipua Rage

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amesema wachezaji Patrick Ochan na Emmanuel Okwi wanamlipua moyo wake kutokana na kucheza soka ya kiwango cha juu.
Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Rage alisema wachezaji hao wawili kutoka Uganda wamekuwa wakiupa raha moyo wake kila wanapokuwa uwanjani wakisakata kabumbu.
Rage alisema katika mchezo wa awali wa michuano ya klabu bingwa Afrika kati yao na TP Mazembe uliochezwa mjini Lubumbashi nchini Congo mwishoni mwa wiki iliyopita, wachezaji hao waliwaduwaza mashabiki wengi waliohudhuria mechi yao.
Alisema baadhi ya watu walioduwazwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu hiyo ni pamoja na viongozi wa TP Mazembe, ambao walikuwa wakiwaulizia mara kwa mara.
"Nilikuwa nimeketi kwenye jukwaa kuu pale uwanjani, kutokana na soka waliyoionyesha, hasa kipindi cha pili, viongozi wa TP Mazembe waliniulizia majina yao,”alisema Rage.
Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, Ochan alikuwa akiwasumbua mara kwa mara mabeki wa timu pinzani kutokana na chenga zake za maudhi, kutoa pasi za uhakika na kuutumia vyema mwili wake, hivyo kuwawia vigumu kumpokonya mpira.
Kwa upande wa Okwi alisema, aliwasumbua sana walinzi wa TP Mazembe na mara nyingi walikuwa wakimchezea rafu kwa lengo la kupunguza kasi yake.
Aliongeza kuwa, ana imani kubwa kwamba Simba ilipoteza mechi ya awali kwa kufungwa mabao 3-1 kwa bahati mbaya kutokana na makosa madogo madogo, ambayo wameshaanza kuyafanyiakazi.
Akizungumzia mechi ya marudiano, Rage alisema tayari maandalizi yameshaanza na kujigamba kuwa, iwe isiwe, lazima TP Mazembe wafungwe kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
"Tumepanga mechi hiyo ianze saa tisa mchana, lengo likiwa ni kuwachosha wachezaji wa TP Mazembe kwa vile jua litakuwa kali. Kule kwao wamezoea hali ya hewa ya baridi,” alisema. Wakati huo huo, baadhi ya wanachama wa klabu ya Simba wa mjini Dar es Salaam wamejigamba kuwa, wameandaa jeneza maalumu kwa ajili ya TP Mazembe kwa vile wana uhakika mkubwa wa kuifunga.
Wanachama hao walisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, wameshaanza kuandaa mbinu za ushindi za nje ya uwanja ili kuhakikisha Simba inaishinda TP Mazembe na kuivua ubingwa wa Afrika.
Kamati ya utendaji ya Simba ilitarajiwa kukutana mwanzoni mwa wiki hii kwa ajili ya kuandaa mikakati ya ushindi. Kikao hicho pia kilitarajiwa kuwahusisha wanachama wa kundi la Friends of Simba.

No comments:

Post a Comment