KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 17, 2011

DEDE: Nimerudi nyumbani


Asema hana kinyongo ama ugomvi na Sikinde
Aliitumikia kwa miaka 21 tangu alipojiunga nayo 1990

MTUNZI na mwimbaji mkongwe wa nyimbo za muziki wa dansi nchini, Shabani dede (54) ametangaza kuihama bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’ na kujiunga na bendi nyingine kongwe ya Msondo Ngoma.
Dede alitangaza uamuzi wake huo juzi, ikiwa ni siku mbili kabla ya bendi hizo zenye mashabiki wengi nchini kufanya onyesho la pamoja kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Mwimbaji huyo mwenye sauti ya mvuto alijiunga na Mlimani Park mwaka 1990 akitokea Msondo Ngoma. Amerejea kwenye bendi hiyo baada ya kuitumikia Sikinde kwa miaka 21.
Akizungumza na Burudani nyumbani kwake Mbagala Rangitatu mjini Dar es Salaam jana, Dede alisema ameamua kurejea Msondo Ngoma baada ya kuikumbuka na kuwakosa mashabiki wake kwa muda mrefu.
Dede, ambaye pia aliwahi kuimbia bendi ya Bima Lee alisema hakushawishiwa na mtu yeyote katika kufikia uamuzi wake huo, ambao alisisitiza kuwa, ulitokana na mapenzi yake binafsi.
“Sikuondoka Sikinde kwa sababu ya kushawishiwa kwa pesa, mtu ama kiongozi yeyote wa Msondo Ngoma. Huu ni uamuzi wangu binafsi,”alisema mwimbaji huyo, ambaye kuna wakati alipachikwa jina la ‘Super Motisha’.
Akifafanua zaidi, alizitaja sababu zingine zilizomfanya afungashe virago Sikinde kuwa ni mapenzi makubwa aliyonayo kwa Msondo Ngoma, bendi ambayo ndiyo iliyomkuza na kumtangaza kimuziki.
Alisema anarudi Msondo Ngoma kwa kishindo hivyo amewataka mashabiki wake wajiandae kusikia nyimbo zake mpya na kali, ambazo tayari ameshazitunga.
Alipoulizwa iwapo ameamua kuondoka Sikinde kwa sababu ya kukosa uongozi, Dede alisema madai hayo si ya kweli kwa sababu hata huko Msondo anakokwenda hana lengo la kuwa kiongozi, bali anataka kuwatumikia mashabiki wake.
“Nimekuwa swahiba mkubwa wa Habibu Mgalusi (kiongozi wa Sikinde) kwa muda mrefu pamoja na wanamuziki wengine, hivyo sina kinyongo ama ugomvi na yeyote. Naitakia kila la heri pamoja na mafanikio mema bendi ya Sikinde,”alisema.
Dede amewataka mashabiki wake wauchukulie uamuzi wake huo kuwa ni wa kawaida kwa mwanamuziki kwa vile katika safari ya kutafuta maisha, lolote linaweza kutokea.
Alitoa mfano wa mwanasoka Mrisho Ngasa, ambaye alipotangaza kuihama Yanga na kujiunga na Azam FC, hakuna aliyepatwa na mshangao kwa sababu ilieleweka kwamba anatafuta maslahi bora zaidi.
Kabla ya kunyakuliwa na Mlimani Park mwaka 1990, Dede aliimbia Msondo Ngoma wakati ilipokuwa chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA) na baadaye OTTU.
Akiwa katika bendi hiyo, Dede alijipatia umaarufu mkubwa kupitia vibao vyake vya ‘Fatuma’, ‘Jenny’, ‘Sauda’, ‘Mkono wa birika’ na nyinginezo. Aliimba nyimbo hizo kwa kushirikiana na marehemu Joseph Lusungu, Juma Akida, Moshi William na Suleiman Mbwembwe.
Dede alijiunga na Msondo Ngoma akitokea bendi ya Dodoma International. Alinyakuliwa kutoka kwenye bendi hiyo na mpiga solo maarufu nchini, Saidi Mabera baada ya kukunwa na kipaji chake cha uimbaji.
Licha ya kujipatia sifa na umaarufu kwa kipindi kifupi, Dede aliamua kuiacha solemba Msondo Ngoma na kujiunga na Sikinde, bendi ambayo ilizidi kumtambulisha zaidi kimuziki. Wakati huo, Sikinde ilikuwa ikimilikiwa na Shirika la Uchumi na Maendeleo la Dar es Salaam (DDC).
Akiwa Sikinde, Dede ambaye aliwahi kushikilia uongozi kwa vipindi vinne tofauti, alitunga nyimbo lukuki, ambazo ziliipatia umaarufu mkubwa bendi hiyo. Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘Talaka rejea’, ‘Amua’, ‘Ndugu wagombanapo’, ‘Kumbuka fadhila’, ‘Binamu’, ‘Uchungu wa mwana’, ‘Chozi la huba’, ‘Fumanizi’, ‘Maneno maneno’ na nyinginezo.
Dede alisema ili kuonyesha uungwana na mapenzi kwa Sikinde, ameamua kuiachia zawadi ya nyimbo zake mbili alizozitunga hivi karibuni. Nyimbo hizo ni ‘Tunu ya upendo’ na ‘Mwanamke akiwezeshwa anaweza’, ambazo zitarekodiwa kwenye albamu mpya ya Sikinde.
Alipoulizwa kuhusu ujio wa Dede, Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti alisema, wanamkaribisha kwa mikono miwili na kuongeza kuwa, watamtambulisha rasmi katika onyesho lao la Jumapili kwenye ukumbi wa Max Bar, Ilala, Dar es Salaam.
Naye Katibu wa Mlimani Park, Hamisi Milambo alisema hawababaiki kuondoka kwa Dede na kwamba wanajipanga upya kuwarejesha waimbaji wao wa zamani, Karama Regesu na Bennovilla Anthony.

No comments:

Post a Comment