KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, March 4, 2011

Dogo Janga achezea kichapo

MSANII chipukizi wa muziki wa kizazi kipya kutoka anga za Arusha, Abdulaziz Abubakar mwishoni mwa wiki iliyopita alipata kichapo kikali kutoka kwa mwalimu wake.
Tukio hilo lilitokea katika shule ya sekondari ya Makongo ya mjini Dar es Salaam, ambako msanii huyo wa kundi la Tip Top Connection anasoma.
Akihojiwa na kituo kimoja cha radio nchini, Abdulaziz, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Dogo Janja alisema, alipatwa na mkasa huo nyakati za mchana baada ya kupishana kauli na mwalimu wake.
Dogo Janja, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza shuleni hapo alisema, tukio hilo lilitokea wakati alipokuwa akienda kupata chakula cha mchana na wanafunzi wenzake.
Kwa mujibu wa msanii huyo, chanzo cha varangati hilo ni kitendo cha mwalimu wake kumwita kwa jina la ‘Dogo Jinga’ na yeye kujibu mapigo kwa kumwita ‘Kubwa Jinga’.
Alisema jibu lake hilo lilionekana kumkera mwalimu wake huyo, ambaye aliamua kumpa kichapo kilichosababisha apatwe na maumivu sehemu za kwenye shingo na mdomo.
Dogo Janja alisema, awali hakuweza kumtambua mtu huyo kwamba alikuwa mwalimu katika shule hiyo kwa sababu ni mgeni na hakuwa na muda mrefu tangu alipoanza kazi.
“Mi nilijua ni mwanafunzi wa vidato vya juu anataka kunizingua, ndiyo maana nikawa namjibu kila alipokuwa ananitukana, mpaka akaamua kunipiga,” alisema Dogo Janja.
Msanii huyo mwenye makeke alisema kwa hali ilivyo, ni bora ahame katika shule hiyo ili kuepuka vipigo zaidi kutoka kwa mwalimu huyo, ambaye amekuwa akimkejeli mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment