KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, March 30, 2011

Studio hii ni ya wote-JK

RAIS Jakaya Kikwete amewataka wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini kuacha malumbano kuhusu umiliki wa studio aliyowafungulia kwa ajili ya kuendeleza vipaji vyao. Kauli hiyo ilitolewa wiki hii na Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Angela Ngowi katika Jukwaa la Sanaa lililofanyika kwenye ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mjini Dar es Salaam. Akizungumza kwa niaba ya Rais Kikwete, Angela alisema ni wajibu wa kila msanii kuelewa kuwa, wote wanaruhusiwa kuitumia studio hiyo kwa kuwasilisha maombi mapema. Angela alisema Rais Kikwete ametoa tamko hilo kwa maandishi, kufuatia kuzuka kwa malumbano miongoni mwa wasanii kuhusu ni nani anayestahili kuisimamia studio hiyo. Akinukuu tamko hilo la Rais Kikwete, Angela alisema: “Nimetoa vifaa vya mastering studio kwa ajili ya wasanii walioomba kwangu kupitia risala, hata hivyo wasanii wote wanaruhusiwa kuitumia na ikiwa kuna yeyote anahitaji, anapaswa kuleta maombi yake.” Tamko hilo lilisababisha mtafaruku kwa baadhi ya wasanii katika jukwaa hilo, akiwemo Mbunge wa Mbeya Mjini (CHADEMA), Joseph Mbilinyi, ambaye alisema wasanii wananyonywa na kutumiwa kisiasa. Mbilinyi alisema ni vyema studio hiyo ingekabidhiwa kwa Kampuni ya Tanzania Fleva Unit bila kupitia BASATA ili iweze kutumiwa na wasanii wote. "Hili suala limeendeshwa kisiasa zaidi, hatutaki kutumika kisiasa, ninashindwa kuelewa ni kwa sababu gani vyombo hivyo visingefikishwa BASATA au vingepitia wizarani," alisema Mbilinyi. "Katika hotuba yake bungeni, Rais Kikwete alisema kuwa kilio cha wasanii amekisikia na sasa tunaambiwa, eti amewapa wale walichokihitaji, sasa mbona hiyo studio hatuioni na tunaambiwa leo amewapa walioomba?" alihoji mbunge huyo. Katibu Mtendaji wa Basata, Ghonche Materego alisema anaheshimu tamko la Rais Kikwete na kuongeza kuwa malumbano kwa wasanii hayana tija. "Nadhani suala ambalo lilikuwa likituchanganya kwa muda mrefu limepatiwa ufumbuzi, hivyo tamko limetolewa tayari na sidhani kama kuna haja ya kuendeleza malumbano," alisema. Msemaji wa Tanzania Fleva Unit, Said Fella, ambaye ndiye aliyewakilisha umoja huo, unaomiliki vyombo hivyo mpaka sasa, alisema waliamua kumuengua Ruge Mutahaba katika usimamizi wa vifaa hivyo kutokana na migogoro iliyokuwa ikiendelea. "Ni muda mrefu tangu tukabidhiwe vifaa hivyo, lakini migogoro ilikuwa haiishi, tuliamua kumuengua Ruge katika usimamizi ili tuweze kufungua studio hii na hivi sasa tumeshasajili kampuni hii Basata" alisema Fela.

No comments:

Post a Comment