KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, March 10, 2011

K-One akamilisha albamu yake mpya

MSANII chipukizi wa muziki za kizazi kipya nchini, Karim Othman amekamilisha kazi ya kurekodi albamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la ‘Sina hakika’.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Karim, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la K-One alisema, albamu hiyo itakuwa na vibao sita, alivyovirekodi kwenye studio za Baucha Records.
K-One alisema amerekodi baadhi ya vibao vyake kwa kuwashirikisha wasanii mbalimbali nyota wa muziki huo kama vile Tundaman, Chegge, Ali Kiba, Madee na Baker.
Alisema ameamua kurekodi na wasanii hao kwa lengo la kuzipa nyimbo zake ladha tofauti na pia kuongeza ushirikiano kati ya wasanii wakongwe na chipukizi hapa nchini.
“Unajua hii ni albamu yangu ya kwanza, hivyo nitakapotoka lazima nitoke kiaina sio kiubabaishaji, ndio maana niliomba kampani ya wakali hawa watano,”alisema.
Alivitaja vibao vitakavyokuwemo kwenye albamu hiyo kuwa ni ‘Ngoja niseme’, ‘Dhahabu’, ‘Nielewe’, ‘Niwaambie’, ‘Weekend special’ na ‘Sina hakika’.
Kwa mujibu wa K-One, albamu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni mwishoni mwa mwezi huu chini ya usimamizi wa Baucha Records.
Msanii huyo mwenye sura ya mvuto alisema pia, tayari ameshatengeneza video ya wimbo wa ‘Sina hakika’, ambao ndio utakaobeba albamu hiyo. Video hiyo imerekodiwa na kampuni ya Showbize.
“Nawaomba mashabiki wangu wakae tayari kunipokea kwa sababu ninakuja kwa mtindo wa aina yake. Nakuja kuwashika,”alisema msanii huyo mwenye maskani yake Kiwalani, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment